Mwanamke Kakamega ajifungua pacha watano kwa mpigo
Na SHABAN MAKOKHA na CHARLES WASONGA
MWANAMKE mwenye umri wa miaka 28 amejifungua watoto watano kwa mpigo katika Hospitali ya Rufaa ya Kakamega.
Bi Everline Namukhula kutoka kijiji cha Shisokhe, kaunti ndogo ya Navakholo alijifungua pacha watano- wavulana wawili na wasichana watatu- mnamo Jumanne usiku kupitia upasuaji.
“Nafurai na natoa shukrani kwa Mungu kwa kunipa watoto hawa watano. Sasa nina jumla ya watoto tisa. Nina wengine wanne na kifungua mimba wangu mwenye umri wa miaka 10 yuko katika darasa la pili,” akasema Bi Nakukhula.
Mumewe ni kiziwe na hufanya kazi za vibarua kijijini humo. Bi Namukhula alisema hataki kupata watoto zaidi kwani huenda akashindwa kubeba gharama ya kuwatunza.
Alisema alipoanza kuhisi uchungu wa kuzaa alienda moja kwa moja hadi katika hospitali ya kaunti ndogo ya Navakholo ambako amekuwa akihudumiwa akitaraji kujifungua mwanawe wa tano.
“Baada ya kuchunguzwa niliambiwa kuwa nilikuwa nimewabeba watoto watatu. Sikutarajia kujifungua watoto watano,” akasema alipoongea na wanahabari kitandani mwake katika kitengo cha kujifungua kina mama.
Kuhamishiwa kwingineko
Alihamishwa hadi Hospitali hiyo ya Rufaa ilipobainika kuwa alikuwa amewabeba zaidi ya watoto watatu.
Dkt Githinji Ndung’u mmoja wa madaktari waliosaidia kujifungua, alisema walimpokea hospitali humo, kutoka hospitali ya kaunti ndogo ya Navakholo mnamo Jumanne.
“Tulilazimishwa kumsaidia kujifungua kupitia upasuaji mwendo wa saa mbili usiku,” akasema Dkt Githinji.
Waziri wa Afya katika kaunti ya Kakamega Rachael Okumu aliahidi kuisajili familia hiyo katika Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Matibabu (NHIF) na kuwalipia ada kwa muda wa mwaka mmoja.