Habari

Muungano wa Wakenya wanaoishi ughaibuni watetea uteuzi wa Bi Mwinzi

June 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

MUUNGANO wa Wakenya wanaoishi Ughaibuni (KDA) unawataka wabunge waidhinishe uteuzi wa Bi Mwende Mwinzi kuwa Balozi wa Kenya nchini Korea Kusini licha ya kuwa na uraia wa mataifa mawili.

Wito huo unajiri baada ya Kamati ya Bunge kuhusu Ulinzi na Mahusiano ya Kigeni kupendekeza jina la Bi Mwinzi lipitishwe pamoja na watu wengine sita lakini baada yake kuasi uraia wake wa Amerika.

Hata hivyo, kwenye barua aliyomwandikia Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Jumatano mwenyekiti wa KDA Dkt Shem Ochuodho anataja msimamo huo kama “ukatili”.

“KDA inachukulia hitaji la kumtaka Mwende kuasi uraia wake wa taifa lingine kama suala ambalo halimhusu yeye pekee bali ni pigo kwa Wakenya wote wanaoishi ng’ambo pamoja na watoto wao waliozaliwa huko,” akasema Ochuodho.

“Wakenya wanaoishi nje na ambao huchangia pakubwa katika ustawi wa Kenya kiuchumi wanapaswa kupewa nafasi ya kuitumikia katika nyanja zote, ndani na nje ya nchi,” akaongeza Bw Ochuodho ambaye alihudumu kama Mbunge wa Rangwe kati ya mwaka wa 1997 hadi 2002.

Muturi haruhusiwi

Lakini Jumatano, Bw Muturi alisema hana uwezo wowote kuhusu suala hilo kwa sababu kulingana na sheria za bunge nambari 122, haruhusiwi kupiga kura wakati wa uamuzi kuhusu suala lolote isipokuwa kusimamia shughuli hizo.

“Sioni haja ya KDA kuniandikia barua kwa sababu kufikia sasa suala hilo liko mbele ya bunge kusubiri uamuzi wa wabunge,” akasema.

“Kamati ilifanyakazi yake na kuandaa ripoti kulingana na sheria za Bunge na Katiba,” Bw Muturi akaongeza.

Haikufahamika ni kwa nini KDA ilifeli kuwasilisha maoni na mapendekezo yake kuhusu kwa njia ya memoranda ikizingatiwa kuwa umma huruhusiwa kufanya hivyo wakati wa shughuli ya kuwapiga msasa watu walioteuliwa kwa nyadhifa za umma.

Ripoti ya kamati hiyo ya Ulinzi na Mahusiano ya Kigeni inayoongozwa na Mbunge wa Kajiado Kusini Katoo Ole Metito iliwasilishwa bungeni Jumanne na itajadiliwa leo Alhamisi, Juni 6, 2019.

Baada ya kujadiliwa wabunge wataamua kuipitisha ilivyo au kuifanyia marekebisho.

Ikipitishwa ilivyo, Bw Muturi ataiwasilisha kwa Rais kwa uteuzi rasmi wa watu hao saba kuwa mabalozi lakini jina la Bi Mwinzi halitachapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali hadi atakapotupilia mbali uraia wake wa Amerika.

Ikiwa ataidhinishwa kwa wadhifa huo kabla ya kukataa uraia wake wa Amerika atakabiliwa na kibarua kikubwa kuamua kuwa mtiifu kwa Kenya au Amerika ikizingatiwa kuwa taifa hilo lina masilahi mengi nchini Korea Kusini.

Dkt Ochuodho anasema kipengee cha 234 (3) cha Katiba kinatambua kati ya balozi na afisa wa kidiplomasia kama maafisa maalum wa umma wenye sifa tofauti na zile za maafisa wa serikali.

Lakini kipengee cha 80 kinalipatia bunge uwezo wa kubuni Sheria kuhusu Uongozi na Maadili kuhusu namna ya kutekeleza hitaji la Sura ya Sita ya Katiba ambalo lafaa kuzingatiwa na maafisa wote wa serikali na wa umma.

Na Sheria ya Uongozi na Maadili inasema mtu aliyeteuliwa kama afisa wa serikali au afisa wa umma hapaswi kuwa na uraia wa mataifa mawili. Na endapo mtu kama huyo atateuliwa sharti aasi uraia wa taifa la pili kabla kuruhusiwa kuchukua wadhifa huo.