Habari

Haji, Kinoti wakana madai kuwa wamekosana

March 5th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

MKURUGENZI wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti na mwenzake wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji wamepuuzilia mbali madai wametofautiana katika utendakazi ilivyoripotiwa katika baadhi ya vyombo vya habari.

Wawili hao waliyataja kama “mambo madogo” wakirejelea kisa ambapo maafisa wa afisi za DPP na wale kutoka DCI walitofautiana mahakamani kuhusu uchunguzi unaoendeshwa kuhusiana na kesi ya ufisadi inayomkabili Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Nchini (KPA) Daniel Manduku.

Mbw Kinoti na Haji walikuwa wakiwahutubia wanahabari Alhamisi katika afisi ya Bw Haji jijini Nairobi.

“Haya madai kwamba nimekosana na mwenzangu Bw Kinoti hayana ukweli wowote. Ni stori zilizotungwa na vyombo vya habari kwa nia mbaya,” akasema Bw Haji.

Akaongeza: “Hatujakosana. Hakuna mzozo wowote kati yangu na DCI wala afisi ya EACC (Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi). Madai hayo yametungwa na watu fulani,” akaongeza.

Bw Haji ambaye alikuwa ameandamana na Bw Kinoti, amewaomba Wakenya kuwa na subira wakati ambapo afisi za DCI na DPP zinachunguza kesi zozote za ufisadi.

Dalili za kuwepo kwa hali ya kutoelewana kati ya wawili hao zilidhihirika Jumatano pale maafisa wa afisi zao walikosa kuelewana kuhusu kukamatwa na kushtakiwa kwa Bw Manduku.

Bw Manduku alikamatwa na maafisa wa DCI Jumatatu na alipaswa kushtakiwa na makosa kadha kuhusiana na sakata ya ufisadi katika KPA.

Hata hivyo, utata ulizuka katika mahakama ya Milimani, Nairobi kwa sababu ya hati ya kumshtaki Bw Manduku ‘kukosekana’.

Mkurugenzi huyo Mkuu wa KPA na Kamishna wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) anayesimamia ushuru wa forodha Kevin Safari waliachiliwa huru baada ya Hakimu Mkuu Kennedy Cheruiyot kubainisha kuwa hakukuwa na hati ya mashtaka yenye majina yao.

“Ikiwa DPP na DCI hawako tayari, hatutaingilia kati bali tutawapa muda waelewane,” Bw Cheruiyot akasema.

Wakati huo huo, Bw Haji ametangaza kuwa afisi yake imefaulu kurejesha Sh385 milioni kama sehemu za mali zilizopatikana kupitia sakata mbalimbali za ufisadi, kama vile ile ya Shirika la Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS).

Amesema pesa hizo ambazo sasa zinahifadhiwa katika benki mbalimbali zitawasilishwa kwa akaunti ya DPP na kisha ziwasilishwe kwa asasi ambako ziliibwa.

Bw Haji amesema Wakenya wanafaa kutarajia mafanikio mengi kutoka kwa afisi za DCI na DPP akisema zinashughulikia kesi nyingi za ufisadi.