Habari

Abdi Guyo amtaka Rais kuingilia uteuzi wa naibu gavana Nairobi

November 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

ALIYEKUWA kiongozi wa wengi katika bunge la Kaunti ya Nairobi Abdi Guyo amemtaka Rais Uhuru Kenyatta kuingilia kati utata uliochangia kutokuwepo kwa mtu wa kuhudumu katika wadhifa wa Naibu Gavana katika Kaunti ya Nairobi.

Bw Guyo ambaye ni diwani wa wadi ya Matopeni amesema ni dhahiri kwamba Gavana Mike Mbuvi Sonko hana nia ya kuteua naibu wake katika siku za hivi karibuni.

“Hii ndiyo maana tunamtaka Rais Kenyatta kuingilia kati suala hili. Sio jambo sawa kwa kaunti kama hii ambayo ndio jiji kuu Kenya kukaa kwa zaidi ya miaka miwili bila Naibu Gavana,” akasema alipofika mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Ugatuzi inayoongozwa na Seneta wa Laikipia John Kinyua.

Akaongeza: “Sioni kama itakuwa rahisi kwa Naibu Gavana kuteuliwa kwa sababu sidhani kuwa Gavana Sonko ana nia ya kufanya hivyo licha ya shinikizo kutoka asasi mbalimbali ikiwemo bunge hili la seneti.”

Bw Guyo alikuwa ameitwa na kamati hiyo kujadili chanzo cha mzozo ambao umekumba bunge la Kaunti ya Nairobi, hali iliyosababisha yeye kupokonywa wadhifa wa kiongozi wa wengi.

Sheria

Itakumbukwa kuwa mwanzoni mwa mwaka 2019 Sonko alisema kuwa hawezi kushurutishwa kuteua naibu gavana kwa sababu hamna sheria inayomshurutisha kufanya hivyo.

“Sheria haijafafanua wazi kwamba sharti niteue naibu gavana. Kwa hivyo, sifai kushurutishwa kufanya kile ambacho sheria haijanilazimu kufanya. Nilimpendekeza Miguna Miguna mapema mwaka huu lakini Spika na madiwani wa Bunge la Kaunti ya Nairobi wakakataa. Juzi nilipokuwa nikitaka kumfanya uteuzi huo, Muungano wa Nasa uliniambia nishauriane nao kwani ulitaka mtu fulani. Kwa kuzingatia moyo wa handisheki niliamua kusimamisha uteuzi huo ili kutoa nafasi kwa mashauriano,” Bw Sonko akaambia kamati hiyo ya Seneti kuhusu Ugatuzi mnamo Aprili mwaka huu.

Suala hilo lilikuwa limeibuliwa na Seneta wa Nairobi Johnston Sakaja ambaye alitaka Bunge la Seneti kuingilia kati kwa kumshinikiza gavana Sonko kuteua naibu wake.

Kiti hicho kimekuwa wazi tangu Januari 2018 baada ya Polycarp Igathe kujiuzulu kwa kile alichodai ni kujuhumiwa na Bw Sonko kwa “kunizuia kuendesha majukumu yangu ya kuwahudumia wakazi wa Kaunti ya Nairobi.”

Wakati huu mswada wa marekebisho ya sheria kuhusu serikali za kaunti unaolenga kutoa mwongozo kuhusu uteuzi wa manaibu wa magavana ungali unashughulikiwa na kamati ya maridhiano yenye wawakilishi kutoka bunge la kitaifa na seneti. Kamati hiyo inasaka muafaka kuhusu mswada huo.