Habari

Abiria walaumu dereva wa basi lililohusika katika ajali iliyoua abiria 10

Na MERCY KOSKEI January 6th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

DEREVA wa basi la Greenline lililohusika katika ajali mbaya Jumapili usiku katika eneo la Karai, Naivasha, Kaunti ya Nakuru, anadaiwa kuendesha gari kiholela, tukio lililosababisha vifo vya watu 10 na kuwaacha wengine kadhaa wakiwa na majeraha mabaya.

Basi hilo liligongana na matatu ya kampuni ya Nanyuki Cab, na kusababisha watu saba kufariki papo hapo, huku wengine watatu wakifariki baadaye walipokuwa wakipokea matibabu katika Hospitali ya Kaunti-ndogo ya Naivasha.

Kulingana na mmoja wa abiria wa basi hilo, Bw Duncan Kirui, aliyepanda basi saa nane mchana Jumapili katika eneo la Wamono, Kaunti ya Bungoma, dereva alikuwa akibeba abiria katika vituo mbalimbali kabla ya kufika Kimilili, ambako safari ilianza rasmi saa kumi jioni.

Bw Kirui alisema kuwa kilomita chache baada ya kuanza safari, dereva ambaye anadaiwa alikuwa amelewa na kutafuna miraa alianza kuendesha kwa kasi, jambo lililowafanya abiria kulalamika kwa makondakta wawili waliokuwemo ndani ya basi.

Kirui, aliyekuwa ameketi kiti nambari mbili, alisema mmoja wa makondakta alijaribu kuzungumza na dereva, lakini dereva akawa mkali na kusisitiza kuwa alikuwa na udhibiti kamili wa gari.

Basi hilo lilisimama kwa dakika 30 jijini Eldoret kabla ya kuendelea na safari, huku dereva akiendelea kuendesha kwa kasi.

“Niliona kila kitu alichokuwa akifanya. Kabla ya kituo chetu cha pili Nakuru, dereva, aliyeonekana kusinzia, alilala kwa muda mfupi. Tuliamka ghafla baada ya basi kugonga shimo. Tulipaza sauti tena tukimuomba kondakta amuonye dereva asimamishe basi apumzike, lakini kilio chetu kilipuuzwa,” alikumbuka.

Kulingana na Bw Kirui, dereva alisimama tena Naivasha ambako abiria kadhaa, akiwemo binamu yake, walishuka. Abiria waliobaki walimlazimisha dereva kwenda katika mkahawa wa karibu ambako alinawa uso kabla ya kuendelea na safari.

“Tulidhani amejirekebisha, lakini alianza tena kuendesha kwa kasi. Tulipofika Karai, gari aina ya Toyota Premio lilikuwa linaingia barabarani kutoka kituo cha mafuta. Basi letu lilikuwa likienda kwa kasi, na licha ya dereva kujaribu kukwepa, aligonga matatu iliyokuwa ikielekea Nakuru. Watu wawili waliokuwa ndani ya matatu waliinusurika lakini wako mahututi. Katika basi letu, mtoto mmoja alifariki na wengine walipata majeraha,” alisema.

Bw Kirui alipata majeraha mguuni na usoni, alitibiwa na baadaye kuruhusiwa kurejea nyumbani.

Alisema alikuwa amesafiri kwenda nyumbani kwa sherehe za Mwaka Mpya na kusema awali, aliwahi kupanda basi lililoendeshwa na dereva huyo huyo ambaye pia alionekana kulewa.

Watu saba, akiwemo dereva na watoto wawili, walifariki eneo la ajali na wengine watatu wakipokea matibabu.

Ajali hiyo ilitokea katika eneo hilo ambapo aliyekuwa Mbunge wa Lugari, Cyrus Jirongo, alifariki wiki chache zilizopita katika ajali kama hiyo.