Habari

Afisa mwingine wa Kenya afa nchini Haiti wengine nane wajeruhiwa

Na CHARLES WASONGA September 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MMOJA wa maafisa wa polisi wa Kenya walioko Haiti kudumisha amani amekufa katika ajali iliyohusisha magari mawili ya kulinda usalama, karibu na jiji kuu Port-au-Prince.

Kwenye taarifa Jumatatu Septemba 1, 2025, msemaji wa Shirika la Kitaifa la Polisi (NPS) Muchiri Nyaga alisema ajali hiyo ilitokea usiku mwendo wa kumi na moja jioni (saa za Haiti) katika barabara ya Kenscoff-Petion-Ville katika eneo la Pelerin 9.

“Kisa hicho kilitokea wakati wa kutolewa kwa magari mawili aina ya MaxxPro. Wakati wa kuburutwa kwa magari hayo, tukio hilo la kisikitisha kilitokea. Raia wengine wawili pia walikufa na maafisa wanane wa kikosi cha kulinda amani Haiti (MSS) wakajeruhiwa,” Bw Nyaga akasema.

“Watatu kati ya waliojeruhiwa wako katika hali mbaya na wanapokea matibabu katika hospital,” akaongeza.

Bw Nyaga alisema kuwa jamaa za polisi wa Kenya aliyekufa wamepashwa habari. Jina lake limebanwa hadi idhini kutoka kwa familia itakapotolewa.

Msemaji huyo wa NPS aliongeza kuwa usimamizi wa kikosi cha walinda amani cha MSS kwa ushirikiano na Polisi wa Kitaifa wa Haiti (HNP), unafanya mipango ya kusafirisha maiti ya polisi huyo nyumbani.

“MSS pia imejitolea kuhakikisha kuwa maafisa waliojeruhiwa wanapata matibabu bora,” Bw Nyaga akaongeza.

Hii sio mara ya kwanza maafa kukumba jumla ya polisi 800 wa Kenya walioko nchini Haiti kwa idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC).

Mwezi Juni mwaka huu afisa kwa jina Samuel Tompoi Kaetua aliuawa katika operesheni ya kiusalama katika aneo la Segur-Savien. Mwili wake ulisafirishwa nyumbani kwa mazishi katika kaunti ya Kajiado.

Polisi hao wa Kenya ni miongoni mwa walinda usalama kutoka mataifa mbalimbali walioko Haiti kupambana na magenge ya wahalifu ili kurejesha usalama nchini humo.

Wakenya hao walipelekwa nchini humo Juni mwaka jana.

Nchi zingine zilizochangia walinda usalama katika kikosi cha MSS ni; Jamaica, Bahamas, Guyana, Barbados, Antigua & Barbuda, Bangladesh, Benin na Chad.

Jumla ya watu 5,500 wameuawa katika mashambulio yaliyotekelezwa na magenge ya wahalifu nchini Haiti mnamo 2024 huku zaidi ya watu milioni moja walitoroka makwao.