Afisa wa bunge anyakwa kwa kudanganya miaka yake ili asistaafu haraka
AFISA mmoja katika Bunge la Kaunti ya Kisii Jumatano asubuhi alifikishwa mahakamani kwa madai ya kughushi cheti chake cha kuzaliwa ili asistaafu haraka.
Inadaiwa David Geoffrey Ombiro, 58, alibadilisha mwaka wake wa kuzaliwa kutoka 1967 hadi 1973.
Akiwa na cheti cha kuzaliwa kilichoghushiwa, alikitumia katika kupata Kitambulisho cha Kitaifa chenye maelezo yaliyokarabatiwa.
Afisa huyo pia anashutumiwa kughushi Nambari ya Kibinafsi ya Mamlaka ya Ushuru wa Kenya (KRA), kadi ya Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Hospitali (NHIF) (sasa haitumiki), na kadi ya Hazina ya Kitaifa ya Hifadhi ya Uzeeni (NSSF) ili kuendana na utambulisho huo potovu.
Kisha aliwasilisha vyeti vilivyobadilishwa kwa Bunge la Kaunti ili kuajiriwa na akafanikiwa katika msako wake wa kazi.
Kufuatia kughushi stakabadhi hizo, Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) ilimfuatilia.
Walimkamata mnamo Jumanne, Septemba 9 na kumhifadhi katika Kituo Kikuu cha polisi cha Kisii kabla ya kufikishwa kortini siku iliyofuata.
Aliwasilishwa mbele ya Hakimu Mkuu Mwandamizi Bernard Omwansa wa Mahakama ya Kisii kujibu mashtaka ya kughushi na kutoa hati za uwongo.
Upande wa mashtaka, ukiongozwa na Solomon Njeru, Victor Kitoto na Stephen Masaki uliambia mahakama kuwa Ombiro alitoa taarifa za uwongo alipokuwa akituma maombi ya kuajiriwa.
“Nyaraka hizi potovu alizowasilisha zilionekana kana kwamba zimetolewa kihalali na mashirika ya serikali kama vile Ofisi ya Kitaifa ya Usajili, Huduma ya Usajili wa Kiraia, Mamlaka ya Ushuru ya Kenya na zingine,” Bw Njeru alisema.
Mshukiwa hata hivyo alikana mashtaka yote na kuachiliwa kwa dhamana ya Sh150,000 na mdhamini mmoja wa kiasi sawa na hicho, au pengine, dhamana ya pesa taslimu Sh70,000.
Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa Septemba 25, 2025.
Kwa siku kadhaa sasa, maafisa hao wa EACC wamekuwa wakichunguza faili za stakabadhi zilizotumiwa na wafanyakazi katika serikali ya kaunti ya Kisii wakati wa kuajiriwa ili kubaini uhalali wao na kukagua dosari zozote. Hii ni baada ya ukaguzi ulioamriwa na Gavana wa Kisii Simba Arati alipochukua mamlaka mnamo 2022.
Mnamo Aprili mwaka huu, aliyekuwa Spika wa Bunge la Kaunti hiyo David Kombo na Naibu Karani David Omwoyo pia walifikishwa mahakamani na EACC.
Wawili hao walilaumiwa kwa matumizi mabaya ya afisi na kumwajiri vibaya afisa wa karani katika Bunge la Kaunti mtawalia.
Walikanusha mashtaka ambayo yalipendekezwa dhidi yao na waliachiliwa kwa dhamana.