Habari

Afisa wa polisi hatarini kuwa kipofu baada ya kupigwa wakati wa maandamano ya Gen Z

Na LEON LIDIGU July 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

BAADHI ya maafisa wa polisi wametoa simulizi za kuatua moyo baada ya kujeruhiwa kutokana na uvamizi wa waandamanaji na wahuni mnamo Juni 25, 2025.

Maandamano ya Juni 25 yalikuwa ya kuadhimisha mwaka moja tangu mauti ya vijana waliotikisa nchi baada ya kufaulu kuvamia Bunge la Kitaifa mwaka uliopita.

Maandamano ya mwaka huu pia yaliishia katika mauaji serikali ikitangaza kuwa Wakenya 10 walifariki japo mashirika ya haki yamesema Wakenya 16 waliangamia.

Afisa wa cheo cha Koplo Charles Kwoba, 42, kwa sasa anapambana asipoteze uwezo wake wa kuona baada ya kupigwa machoni wakati wa maandamano hayo.

Bw Kwoba amefanyiwa upasuaji mara mbili machoni ambao umegharimu zaidi ya Sh1 milioni. Afisa huyo kutoka Kituo cha Kikuyu Kaunti ya Kiambu na wenzake walijipata katikati ya waandamanaji eneo la Kikuyu na akapigwa kwa mawe usoni.

“Siku hiyo niliona kifo kimenijia na macho yangu ya kulia yamekuwa yakisumbua sana, naona tu giza. Daktari anasema kuwa machozi na damu zimejaa na kuganda na lazima ziondolewe kwa dharura,” akasema Bw Kwoba akitokwa na machozi.

Akionekana mwenye huzuni, Bw Kwoba baba ya watoto sita anasikitika kuwa madaktari wamemwambia ana kati ya asilimia 30 na 40 ya kuona tena.

Bw Kwoba anakiri kuwa siku hiyo walilemewa na waandamanaji katika soko la Ndonyo, Dagoretti mjini hata baada ya kupigwa jeki na wenzao kutoka kituo cha polisi cha Karen.

Alisema kuwa vijana waliwalemea na mkuu wa kituo chao cha polisi aliomba msaada kutoka kwa vituo vingine. Baadaye walielekezwa katika eneo la Kikuyu ambapo mahakama ilikuwa ikiteketezwa na kituo cha polisi kuvamiwa.

Alipotoa helmeti au kofia ya chuma aliyovaa, alipatwa na jiwe kwenye macho na akapoteza fahamu. Kilichosikitisha zaidi ni kuwa zaidi ya waandamanaji 5,000 walitishia kuteketeza Hospitali ya Lifecare Kikuyu na ikabidi atolewe kisiri na kurejeshwa kituoni.

Alikaa kituoni kwa siku nne bila kupokea msaada ndipo rafikiye Moses Ngui akampeleka Hospitali ya macho ya Lions SightFirst ambako amekuwa akigharimia matibabu yake kwa kuwa bima ya polisi haitoshi.

“Nimekuwa afisa wa polisi tangu mnamo 2006 na kuyashughulikia maandamano mengi. Chuki na hasira zilizoonyeshwa na waliokuwa wakitupa mawe ilisikitisha sana,” akasema Bw Ngugi.