Afisa wa zamani wa KDF asukumwa ndani
ALIYEKUWA afisa wa Jeshi (KDF) atazuiliwa kwa siku saba kuhojiwa na maafisa wa uchunguzi wa jinai (DCI) baada ya madai kwamba alikuwa anapa makrutu barua za kuanza mafunzo ya kijeshi.
Hakimu mkuu mahakama ya Milimani Lucas Onyina aliamuru Joshua Mutwii Maingi azuiliwe katika kituo cha Polisi cha Muthaiga kwa siku saba.
Bw Onyina alitoa agizo hilo baada ya kiongozi wa mashtaka kumsihi amzuilie Maingi kuhojiwa kuhusu mabarua ya ajira aliyokuwa anawapa makrutu.
Hakimu alifahamishwa na afisa anayechunguza kesi hiyo Bw Wilson Kamundi kwamba mshukiwa huyo aliwataka wenye kupokea mabarua ya ajira wafike katika shule ya kutoa mafunzo ya kijeshi (RTS) Eldoret Novemba 17,2025.
Mahakama ilifahamishwa baada ya polisi kupata habari kumuhusu mshukiwa makachero walimwandama hadi katika makazi yake eneo la Kilimani, Nairobi.
“Mshukiwa huyo alipatikana amevalia sare za Jeshi la Angani akiwa ndani ya makazi yake Kilimani,” Bw Kamundi alieleza mahakama.
Polisi walipata mabarua ambayo mshukiwa alikuwa ameandikia makrutu na kuwataka wafike RTS Eldoret mara moja.
“Tulipokuwa tukiendelea na mahojiano tulipokea simu kutoka kwa Brenda Chepkorir akidai alikuwa amemtumia Maingi Sh510,000 amsaidie kujiunga na Jeshi la Nchi Kavu (KA),” Bw Kamundi alimweleza hakimu.
Afisa huyo wa DCI alieleza mahakama kwamba polisi walitwaa sare hizo za KDF makao makuu kijeshi (DoD) kubaini ikiwa ni halali za kijeshi ama zimeshonwa na fundi wa jua kali.
“Hatujui DoD itachukua muda kiasi kipi kubaini sare hizo. Twahitaji muda pia kumhoji mshukiwa,” alisema Bw Kamundi.
Mahakama ilijuzwa watamsaka Bi Chepkorir aandikishe taarifa.
Akitoa uamuzi Bw Onyina alisema ombi la upande wa mashtaka liko na mashiko kisheria kisha akaamuru mshukiwa huyo azuiliwe katika kituo cha polisi cha Parklands.
Hakimu aliagiza kesi hiyo itajwe Novemba 24,2025.