Afisi ya Rais Ruto yataka iongezwe Sh651 milioni zingine kwenye bajeti
AFISI ya Rais sasa inataka Sh651 milioni zaidi kulipa mishahara ya wafanyakazi, kufadhili shughuli za Baraza la Kitaifa la Usalama na kulipa wawasilishaji bidhaa.
Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei amesema bajeti ya Afisi ya Rais huwa ni kidogo na hailingani na gharama ya mipango mbalimbali inayotekelezwa.
Kutokana na bajeti ndogo, afisi hiyo haiwezi kutimiza wajibu wake wa kutoa uongozi bora kwenye utumishi wa umma na kuendeleza mipango ya serikali jinsi ambavyo inatakikana.
Bw Koskei jana aliambia Kamati ya Utawala na Usalama wa Ndani kuwa afisi hiyo haina mgao wa bajeti inayoelekezwa kwenye miradi ya maendeleo kwa kuwa pesa hizo zilitumika kwenye bajeti ya awali na ya ziada.
“Katika mwaka wa kifedha wa 2024/25 bajeti ya pili ya ziada, afisi ya Rais inahitaji Sh651.68 milioni ambapo Sh601.8 milioni zitatumika kulipa mishahara na matumizi mengine kisha Sh50 milioni kwamaendeleo,” Bw Koskei akaambia kamati hiyo.
Alisema Sh70.65 milioni zitatumika kwenye huduma za kichapishi na kuwalipa marupurupu wafanyakazi ambao walikuwa kazini kwa zaidi ya muda uliowekwa kisheria.
Aidha Sh498 milioni imetengewa kulipa wafanyakazi katika afisi mbalimbali chini ya Afisi ya Rais na Msemaji wa serikali. Aidha Afisi ya Rais inataka Sh105 milioni itengewe Bodi inayosimamia Makavazi, Sanaa, Michezo kuiwezesha kutekeleza wajibu wake ipasavyo.
Bw Koskei alisema Afisi ya Rais imekuwa ikipokea mgao mdogo kwenye idara zake mbalimbali na imelemewa kupata Sh382.29 milioni kulipa wawasilishaji bidhaa.
Alisema afisi hiyo inataka Sh213.59 milioni kulipa marupurupu ili kulipa Jopo la Habari la Serikali liliongozwa na Jaji Kullow, kulipia shughuli ya jopo lililowateua Makamishina wa Tume ya Utumishi wa Umma na kulipa marupurupu ambayo hayakuwa yamelipwa.
Afisi ya Mkuu wa Wafanyakazi Ikulu na Mtumishi wa Umma zinahitaji Sh200 milioni kununua magari. Hii ni kwa sababu afisi hizo mbili zimekuwa zikitumia magari nzee, yaliyochakaa ambayo ni gharama kubwa kutengeneza kila mara.
“Kwa hivy0, afisi hizo zinahitaji Sh200 milioni kuyanunua magari mapya,” akasema Bw Koskei mbele ya kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Narok Magharibi Gabriel Tongoyo.
Mradi wa upanzi wa miti bilioni 15 nayo ina mwanya wa ufadhili wa Sh100 milioni. Afisi ya Rais huwa ina malengo ya kupanda miti milioni 50 kila mwaka na Bw Koskei alisema pesa hizo zinahitajika kulipa mbegu na shughuli za upanzi wa miti.
Mkuu huyo wa utumishi wa umma alisema Mkurugenzi wa Uwiano wa Kitaifa anahitaji Sh70 milioni kuandaa ripoti ya kila mwaka kuhusu maadili na sheria za uongozi kwa mujibu wa katiba ya 2010.
“Kwa jumla Afisi ya Rais ina upungufu kwenye idara mbalimbali na inahitaji bajeti ya Sh3.048 bilioni. Afisi hii inaomba kamati hii itathmini kuiongezea mgao zaidi kushughulikia masuala yaliyoibuliwa,” akasema Koskei.