Afrika yasimama na Mugabe
Na WANDERI KAMAU na MASHIRIKA
VIONGOZI mbalimbali barani Afrika waliungana Ijumaa kumwomboleza aliyekuwa rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, wakimtaja kama mzalendo na shujaa wa ukombozi.
Mugabe alifariki katika hospitali moja nchini Singapore, alikokuwa akipokea matibabu.
Viongozi wa mataifa kutoka pembe zote za Afrika walimmininia sifa Mugabe huku Rais Uhuru Kenyatta akitangaza siku tatu za maombolezo kote nchini.
Rais Kenyatta pia aliagiza taasisi zote za umma na kijeshi kupeperusha bendera nusu mlingoti kutoka leo hadi Jumatatu jioni kwa heshima ya Mugabe.
Na huku bara la Afrika likimsifu, mataifa ya Ulaya na Amerika yalimtaja kama dikteta kwa sababu ya misimamo yake mikali kupinga ukoloni mamboleo.
Kwenye ujumbe wake wa rambirambi, Rais Kenyatta alimtaja Mugabe kama rafiki wa karibu wa Kenya, aliyeshiriki sana katika harakati za kulikomboa bara Afrika kutoka kwa minyororo ya ukoloni.
“Kenya imempoteza rafiki wa karibu. Nachukua fursa hii kuifariji familia ya Bw Mugabe, hasa mkewe, Grace Mugabe na raia wote wa Zimbabwe. Bw Mugabe alikuwa nguzo kuu kwenye harakati za ukombozi wa Afrika. Alitumia muda wake mwingi kuishinikiza Afrika kutambua nafasi na sauti yake duniani,” akasema Rais Kenyatta.
Wengine waliomwomboleza ni marais wastaafu Daniel Moi na Mwai Kibaki, Naibu Rais William Ruto, kiongozi wa ODM Raila Odinga kati ya wengine.
Kwenye ujumbe wake, Bw Moi alimtaja Bw Mugabe kama mpiganiaji ukombozi, atakayekumbukwa na vizazi vijavyo. Bw Moi alikumbuka jinsi marehemu alitumikia vifungo virefu gerezani, akipigania ukombozi wa Zimbabwe, wakati huo ikifahamika kama Rhodesia.
“Akiwa na viongozi wenzake kama Joshua Nkomo, Leopold Takawira, James Chikerema na Ndabaningi Sitole, Mugabe alifanikiwa kuukabili na kumaliza utawala wa kikoloni ulioongozwa na Ian Smith,” akasema.
Msingi wa uongozi
Bw Kibaki, alisema kuwa, kifo cha Bw Mugabe kinafikisha mwisho enzi ya viongozi walioshiriki kuweka msingi wa uongozi barani Afrika.
Dkt Ruto alimtaja Mugabe kama shujaa aliyeshiriki katika vita vya ukombozi wa Zimbabwe kwa kujitolea kuona kuwa Waafrika wamekuwa huru.
Bw Odinga naye alisema kuwa huu ni wakati muhimu kwa raia wa Zimbabwe kutathmini safari yao kama taifa huru na njia za kuifanya kuwa nchi inayostawi kimaendeleo.
Viongozi wengine waliomwomboleza ni Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, John Magufuli wa Tanzania, Muhammadu Buhari wa Nigeria, Botwana, Uchina kati ya nchi zingine.
Rais Buhari alisema kujitolea kwa Mugabe kupigania uhuru kutakumbukwa na raia wa Zimbabwe vizazi vingi vijavyo.
Lakini Uingereza iliisema kuwa kifo chake “kitazua hisia mseto.”