Habari

Afueni kwa raia, pigo kwa wabunge Rais kukataa kutia saini mswada wa PSC

September 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

WALIPA ushuru wamepata afueni kubwa baada ya Rais Uhuru Kenyatta kudinda kutia saini mswada ambao ungewapa wabunge uwezo wa kujipatia marupurupu ya juu.

Wabunge walikuwa wamepenyeza kipengee katika Mswada wa Tume ya Huduma za Bunge (PSC) wa 2018 na hivyo kuipa uwezo tume hiyo kuwaongezea marupurupu ya usafiri humu nchini na katika mataifa ya nje bila kuhusisha Tume ya Kukadiria Mishahara na Marupurupu ya Watumishi wa Umma (SRC).

Mswada huo pia uliipa PSC mamlaka ya kukadiria kiwango cha marupurupu ambacho wabunge na maseneta wangekuwa wakipokea wanaposafiri nje ya Nairobi kwa shughuli zinazohusiana na majukumu yao.

Rais Kenyatta alirejesha mswada huo katika bunge huku akiuandamanisha na memoranda kuhusu sehemu ambazo zinapafaa kufanyiwa mabadiliko.

“Kwa kutumia mamlaka niliyopewa na kipengee cha 115 (1) (b) cha Katiba, nimekataa kutia saini Mswada wa Tume ya Huduma za Bunge (PSC) wa 2018 kutokana na sababu nilizoeleza katika memoranda hii,” Rais akasema kwenye taarifa aliyotuma kwa Afisi ya Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi.

Rais aliwataka wabunge kuondoa kipengee cha 20 cha mswada huo kinachoipa PSC mamlaka ya kufanyia mabadiliko marupurupu yao, na wafanyakazi wengine wa bunge; ya usafiri humu nchini na kimataifa bila kusaka ushauri kutoka SRC.

Kulingana na kipengee hicho, PSC ina mamlaka ya kuongeza marupurupu hayo “kila wakati haja inapotokea bila kushauriana na SRC”.

Asasi yenye mamlaka

Rais Kenyatta aliwaambia wabunge kwamba SRC ndiyo asasi ya kipekee yenye mamlaka ya kukadiria kiwango cha mishahara na marupurupu yote ya maafisa wote wakuu wa serikali. Katiba inachukulia wabunge kama maafisa wakuu wa serikali.

Kiongozi wa taifa pia aliamuru kwamba bunge lifute kipengee cha 43 ya mswada huo kinacholenga kuipa PSC mamlaka ya kukadiria mishahara na marupurupu ya wabunge na mafanyakazi wa bunge.

Sheria hiyo ililenga kuimarisha uwezo wa wabunge kuitisha nyongeza ya mishahara kila mara wanapotaka kwa sababu baadhi yao ni wanachama wa tume.

Isitoshe, Spika Muturi ndiye mwenyekiti wa PSC huku afisa mkuu mtendaji akiwa Karani wa Seneti Jeremiah Nyengenye.

Mswada huo ungetiwa saini, wabunge wangekuwa na haki ya kupokea marupurupu kadhaa kama vile Sh250,000 za nyumba na kati ya Sh18,000 hadi Sh24,000 kama marupurupu ya malazi wakiwa Nairobi.

Wabunge pia walikuwa wamependekeza kuwa wapewa huduma bora inavyopewa wabunge kutoka mataifa mengi yaliyoendelea kiuchumi.

Kama ungepitishwa kwa Rais kutia saini, wabunge na maseneta wangegharimiwa huduma kama vile chumba cha wageni katika afisi zao, watafiti, huduma za Intaneti na chumba maalum cha makundi ya wabunge wa vyama mbalimbali kukutana.

Pia wanataka wabunge wawe wakipewa mafunzo kila mara humu nchini na ng’ambo.

Aidha, walitaka wajengewe duka maalum ambako watakuwa wakinunua bidhaa mbalimbali pamoja na zawadi. Vilevile, walitaka mtaalamu wa afya aajiriwe bungeni kuwapa huduma maalum.

Wabunge sasa wana kibarua kigumu cha kubatilisha mapendekezo kwenye memoranda ya Rais kwani wanahitaji kufanya hivyo kupitia upigaji kura wa angalau thuluthi mbili ya wabunge wote. Hii ni sawa na wabunge 233 kati ya 349.