Afueni kwa watayarishaji wa makala ya uchunguzi ya Blood Parliament
MAHAKAMA yaongeza muda wa kusimamisha kukamatwa kwa watayarishaji filamu wanne wa Kenya hadi uchunguzi utakapokamilika.
Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) amesema kuwa uchunguzi wa polisi haujakamilika hivyo hakuna mashtaka dhidi yao.
Nicholas Gichuki, Brian Adagala, Mark Denver Karubiu na Chris Wamae walikamatwa mnamo Mei 2, 2025 usiku na kuzuiliwa katika vituo vya polisi vya Pangani na Muthaiga.
Baada ya kukamatwa kwao, wakili wao walidai kuwa mahojiano na polisi ionyesha walikuwa wakijaribu kuwahusisha na makala ya BBC Africa Eye: Blood Parliament.
Hata hivyo, BBC ilisema kwamba vijana hao hawakuhusika kwa vyovyote kutayarisha makala hayo.
“Tumefahamishwa kuhusu kukamatwa kwa wanahabari wanne nchini Kenya. Ili kuwa wazi, hawakuhusika kwa njia yoyote kutayarisha makala ya BBC Africa Eye: Blood Parliament,” ilisema ofisi ya habari ya BBC katika taarifa.
Makala hayo yaliwataja maafisa kadhaa wa usalama wanaodaiwa kuhusika moja kwa moja na mauaji ya waandamanaji wasiokuwa na silaha.
Wanne hao waliachiliwa Jumamosi, Mei 3, kufuatia kilio cha umma kuhusu kukamatwa kwao.