Afueni SGR ikirejelea safari zilizofutwa kutokana na maandamano
WASAFIRI kutoka Mombasa hadi Nairobi kupitia reli ya kisasa ya SGR waliondoka Nairobi saa nne asubuhi, saa 12 baada ya Shirika la Reli Nchini (SGR) kusitisha safari yao ya kuja Nairobi saa nne usiku wa Jumapili.
Kusitishwa kwa safari hiyo dakika ya mwisho, kulisababisha wengi wakwame katika kituo cha reli cha Mombasa.
Mapema Jumapili, wasafiri wengine kutoka Kaunti ya Kwale pia walikosa treni yao ya saa tisa mchana baada ya polisi kuweka kizuizi kwenye barabara ya Dongo Kundu.
Shirika la Reli baadaye lilitoa taarifa saa sita na nusu Jumatatu na kuwashauri wale ambao safari zao zilifutwa wafike katika kituo cha SGR saa mbili asubuhi.
Shirika hilo lilihusisha kufutiliwa kwa safari hizo na tatizo la kiufundi.

“Tumefanya juhudi za kuhakikisha kuwa abiria wote walioathirika ikiwemo wale ambao walikosa treni wanasafiri,” ikasema taarifa ya Shirika hilo na kusema tikiti za Julai 6 bado zingetumika.
Bi Wambui Gathu ambaye alikuwa asafiri hadi Nairobi alisema alitoka Diani Kaunti ya Kwale Jumapili mchana.
“Sasa sijui nitaenda wapi kwa sababu nimeudhika na pia nimehangaika sana. Kinachoudhi zaidi ni kuwa hakukuwa na taarifa za mapema za kutuambia kuwa safari ingeahirishwa,” akasema Bi Wambui Jumapili usiku.
Msafiri mwengine Emmanuel Koech naye alilalamikia hatua ya kusitishwa kwa safari bila maslahi ya umma kuangaziwa.
“Mbona wanahofu? Mbona watuadhibu hivi? Hata sisi ni walipaushuru na hatufai kufanyiwa hivi,” akasema Bw Koech.
Baadhi ya wasafiri waliamua kupata hasara na kutumia basi kwa kuwa mabasi yalijaa kwenye kituo hicho cha reli baada ya kupata habari safari ziliahirishwa.