Aga Khan azikwa kishujaa nchini Misri
MWANAMFALME Karim Al-Hussaini Aga Khan IV, ambaye ni Kiongozi wa 49 wa Waislamu wa dhehebu la Shia, Ismaili Jumapili alizikwa kishujaa kwenye hafla ya kibinafsi Aswan, Misri.
Aga Khan ni mwanzilishi na mdhamini wa Shirika la Aga Khan Development Network (AKDN) na mwanzilishi wa Nation Media Group inayomiliki Taifa Leo.
Mazishi yake yalifanyika siku tano baada ya mauko yake Februari 4, jijini Lisbon, Ureno akiwa na umri wa miaka 88.
Mwanawe na mrithi Mwanamflame Rahim Aga Khan V tayari ametajwa Kiongozi wa 50 wa Waislamu wa Shia Ismaili, alihudhuria mazishi hayo pamoja na wanafamilia, viongozi na umma wa Ismailia.
“Gavana wa Aswan, kama ishara ya heshima, aliungana na msafara uliobeba mwili wa marehemu hadi kando mwa mto Nile. Jeneza la marehemu Karim Aga Khan IV lilihamishwa hadi kwenye boti hadi eneo tengwa ambapo miili ya Villa Nour El Salaam na Aga Khan III ilizikwa,” ikasema taarifa kutoka Diwan wa Ismaili Imamat.
“Jeneza lilibebwa kwa mkono kwenye msafara huo ulioongozwa na wanafamilia. Mwili wa Muadhamu ulizikwa kwenye makaburi hayo ambayo yapo kwenye kilele cha mlima ukiangalia mto Nile.”
Hafla hiyo iliendeshwa kwa tamaduni ya Kiislamu na baada ya mazishi Gavana wa Aswan Meja Jenerali Ismail Kamal alimpa Mwanamfalme Aga Khan V na ufunguo wa jiji la Aswan kama ishara ya heshima.
Kufuatia kuaga kwa babake Lisbon, Ureno, Mwanamfalme Rahim alichukua usukani kwa mujibu wa tamaduni wa Shiam Imami Ismaili.
Misri ina umuhimu mkubwa sana kwa jamii ya Ismaili kwa kuwa ni kitovu cha Fatimid Caliphate ambacho kilikuwa kikiongozwa na Maimamu Ismaili kwenye karne ya 10 na 11 mtawalia.