Habari

Ahadi hewa ya Duale: Hospitali ya St Mary’s Mumias bado haijafunguliwa licha ya ahadi ya serikali

Na LEON LIDIGU na SHABAN MAKOKHA November 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

LICHA  ya tangazo la Waziri wa Afya Aden Duale mnamo Agosti kwamba Hospitali ya St Mary’s Mumias imefunguliwa tena, ukweli ni kwamba hospitali hiyo ya miaka 93 inayomilikiwa na Kanisa Katoliki bado imefungwa.

Kulingana na Padri Ian Kafuna, kasisi wa Kanisa Katoliki la St Peter’s Mumias na msimamizi wa hospitali hiyo, deni la Sh180 milioni ambalo serikali kupitia Hazina ya Kitaifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) inadai kulipa, bado halijaingia kwenye akaunti ya hospitali.

“Tunaamini serikali ina nia njema ya kufufua hospitali hii, ingawa ucheleweshaji haupukiki. Tuna matumaini fedha hizo zitafika,” alisema Padri Kafuna.

Tangu kufungwa kwake mnamo Juni 3, mamia ya wagonjwa na kina mama wajawazito wamekuwa wakisafiri hadi Butere, Matungu na Kakamega kupata huduma za afya. Uongozi wa hospitali ulifunga milango ukitaja mrundiko wa madeni kutokana na madeni ambayo NHIF na SHA hazijalipa.

Seneta wa Kakamega Boni Khalwale alisema amekuwa akituma maombi kwa SHA kutuma fedha hizo na sasa atalazimika kuwasilisha hoja bungeni kuokoa hospitali hiyo.
“Nitapeleka ombi bungeni kuhusu suala hili. Tukichelewa, wakazi wa Kakamega na kaunti jirani wanaotegemea hospitali hii wataipoteza kabisa,” alisema Khalwale.

Katika hafla ya Agosti 3, wakati wa kuzindua mpango wa TaifaCare huko Kakamega, Waziri Duale akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa SHA Mercy Mwangangi walitangaza kuwa hospitali imefunguliwa na kwamba serikali ingetuma Sh14 milioni ili ianze shughuli.
Duale alidai serikali ilikuwa umelipa nusu ya deni iliyodaiwa na hospitali hiyo.

Hata hivyo, Askofu Joseph Obanyi alisema serikali bado inadaiwa Sh35 milioni.
“Serikali ilikuwa inadaiwa Sh140 milioni kutoka NHIF na Sh40 milioni kutoka SHA. Kufikia sasa tumepokea Sh98 milioni pekee,” alisema Askofu Obanyi akimwomba Rais William Ruto kuingilia kati.

Hata hivyo, Oktoba 25, Waziri Duale aliambia Seneti kwamba suala la St. Mary’s “linatumiwa kisiasa.”
“Niliketi na Askofu Obanyi na timu nzima pamoja na meneja wa benki, tukathibitisha kuwa tumelipa Sh90 milioni, na Sh14 milioni zilizokuwa zimebaki pia tumelipa. Kwa hivyo waulizeni wao kwa nini hospitali haijafunguliwa,” alisema Duale.

Aliongeza: “Nilisema tusitumie St. Mary’s kwa siasa. Watu wa Kakamega wananitazama. Mimi nilifanya sehemu yangu, kama usimamizi umeamua kufunga hospitali, hilo halinihusu mimi.”

Lakini alipoulizwa tena na Taifa Leo Dijitali siku ya Alhamisi, Oktoba 30, 2025, Askofu Obanyi alisema hana habari kuhusu malipo hayo kwa kuwa hahusiki tena na usimamizi wa kila siku wa hospitali.
“Naomba uwasiliane na wasimamizi wa St. Peter’s Mumias wanaoshughulikia mambo ya kila siku,” alisema huku akisisitiza kuwa deni hilo bado halijalipwa.