AI kutumika kuteua wanafunzi wa Gredi 9 kujiunga na Sekondari
WIZARA ya Elimu imeanzisha mfumo mpya wa kidijitali wa kuchagua wanafunzi wa Darasa la 9 watakaojiunga na shule za sekondari pevu chini ya mfumo wa elimu unaozingatia umahiri (CBC).
Mfumo huo unalenga kuhakikisha haki, usawa, na uwakilishi wa kitaifa katika mchakato wa kwanza wa kuwateua wanafunzi hao, ambao unatarajiwa kufanyika baada ya mtihani wa Kenya Junior School Education Assessment (KJSEA) utakaoanza Jumatatu ijayo.
Kundi hili la kwanza lina zaidi ya wanafunzi milioni 1.13 ambao watapangwa kwa misingi ya utendakazi wao, mkondo wa masomo, na nafasi kwa kuzingatia kila kaunti.
Mfumo huo wa kidijitali, ambao kwa sasa uko katika awamu ya majaribio, utatumia Akili Unde ili kuwezesha uteuzi wa haki kwa wanafunzi wote kutoka kila kona ya nchi.
Kwa mujibu wa Katibu wa Elimu ya Msingi, Profesa Julius Bitok, shule zimegawanywa katika makundi manne.
Kundi la 1 ni shule za kitaifa zenye miundombinu bora na uwezo wa kutoa mikondo mitatu ya, kundi la 2 ni shule za mikoa, kundi la 3 ni shule za kaunti, na kundi la 4 ni shule za kutwa au kaunti ndogo.
Prof Bitok alisema angalau mtoto mmoja kutoka kila mojawapo ya kaunti 47 atapata nafasi katika shule ya Kundi la 1.
Hii inafanikishwa na mfumo wa kidijitali unaohakikisha usawa na uwakilishi wa kitaifa.
Aliongeza kuwa mfumo huo utawezesha mwanafunzi kutoka maeneo kama Mandera kujiunga na shule zilizoko Kisumu, au mwanafunzi kutoka Mombasa kujiunga na shule ya Nairobi, katika kuimarisha mshikamano wa kitaifa kupitia elimu.