Ajipeleka kwa polisi baada ya kuua wakizozania kumbikumbi
Na ALEX NJERU
ILIKUWA ni huzuni na simanzi katika kijiji cha Kamatungu mjini Marimanti, Kaunti ya Tharaka-Nithi baada ya mwanamume kumuua mwenzake kwa kisu kufuatia mzozo kuhusu kumbikumbi.
Muriungi Kiyogere, 35, anadaiwa kumdunga kisu mara nne Daniel Mutiria Cece aliyekuwa na umri wa miaka 36 ambaye hufanya kazi ya juakali mjini Marimanti mnamo Jumapili jioni.
Akithibitisha kisa hicho, Kamanda wa Polisi wa Tharaka Kusini, Kiprop Rutto alisema mshukiwa alitorokea katika Kituo cha Polisi cha Marimanti kuwahepa wanakijiji waliokuwa wakitaka kumuua.
“Mshukiwa alitoroka alipogundua kuwa wanakijiji waliokuwa na hasira walikuwa wakimsaka. Alipofika kituoni alikiri kumuua mwendazake,” akasema Bw Rutto.
Mshukiwa alizuiliwa kituoni hapo na maafisa wa polisi wakakimbia katika eneo la tukio ambapo walipata mwili wa mwendazake ukiwa umeloa damu.
Bw Rutto alisema uchunguzi wa mwanzoni unaonyesha kuwa mzozo baina ya wawili hao ulizuka baada ya mwendazake kumpata mshukiwa akiokota kumbikumbi karibu na mlango wa nyuma yake.
Mwendazake, kulingana na polisi, alimtaka mshukiwa kumkabidhi kumbikumbi hao huku akisisitiza kuwa walikuwa wake.
Arejea akiwa amejihami kwa kisu
Walianza kupigana na hapo ndipo mshukiwa akawahi katika nyumba yake na kurejea akiwa na kisu na kumshambulia mwendazake.
Kulingana na mashahidi, mshukiwa na mwendazake wamekuwa marafiki kwa miaka mingi na walikuwa wakibugia pombe pamoja Jumapili.
“Tulishtushwa mno na unyama huo kwani hatujawahi kushuhudia kitendo cha aina hiyo katika eneo hili,” akasema Bi Jane Muthoni.
Bw Jacob M’Chabari, mmoja wa wazee wa baraza la Njuri Ncheke, alisema kuwa ni mwiko kwa wanaume waliotahiriwa kula kumbikumbi katika jamii ya Wameru.
M’Chabari alisema kuwa kumbikumbi wanaruhusiwa kuliwa na wanawake pamoja na watoto.