Akana kuiba tikiti za ndege za Sh4.1M
MFANYAKAZI wa zamani wa kampuni ya usafiri aliyetiwa nguvuni akienda nchini Uturuki ameshtakiwa kwa wizi wa tikiti za ndege za thamani ya Sh4.1milioni miaka sita iliyopita.
Carolyne Wanjiru Munene alikamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA).
Alimsihi hakimu mkuu mahakama ya Milimani Nairobi Lucas Onyina amwachilie kwa dhamana isiyo ya kiwango cha juu mno.
Wanjiru aliungama kwamba hakuwa akitoroka ila alikuwa anasafiri kuhudhuria warsha ya kibiashara ya kimataifa nchini Uturuki.
Wanjiru aliambia korti atazingatia masharti atakayopewa ya dhamana.
Upande wa mashtaka haukupinga mshtakiwa akiachiliwa kwa dhama ila hakimu aliombwa azingatie kiwango cha pesa anachodaiwa kuiba.
Shtaka dhidi ya Wanjiru lilisema aliiba Sh4.1milioni kati ya Novemba 12,2019 na Januari 9,2020 akiwa mfanyakazi wa kampuni ya African Touch Safaris Limited (ATSL) yenye afisi zake jengo la ACK Garden House jijini Nairobi.
Hakimu alielezwa mshtakiwa aliiba tikiti za ndege 21 zenye thamani ya Sh4,127,820.
Mahakama iliambiwa mshtakiwa alipokea tikiti hizo kutokana na cheo chake kazini.
Aliachiliwa kwa dhamana ya Sh500,000 pesa taslimu.