Makala

AKILIMALI: Abuni mbinu safi ya kuivisha maembe haraka

December 24th, 2020 3 min read

PIUS MAUNDU na CHARLES WASONGA

KILIMO cha maembe ndio tegemeo kwa wakazi wengi wa kaunti ya Makueni ambao mara nyingi huzongwa na changamoto ya ukame.

Kulingana na takwimu kutoka kwa Wizara ya Kilimo zaidi ya watu 109,465 hukuza na kuuza matunda haya kupitia vyama vya ushirika au kwa njia ya reja reja.

Kando na kuuzwa sokoni kwa wateja wanaoyala yakiwa mbivu, kuna maembe pia huongezwa thamani kupitia utayarishaji wa sharubati (juisi).

Hii ndio maana mradi wa kutengeneza juisi ya maembe kwa jina “Kalamba Fruit Processing Plant” ulioanzishwa na Serikali Gavana Profesa Kivutha Kibwana ni muhimu zaidi kwa wakulima wa zao hili.

Msimu wa mavuno wa maembe huanza mwezi wa Januari na kukamilika mwezi wa Machi kila mwaka wakati ambapo bei ya matunda hayo hushuka zaidi.

Wengi wa wakulima hulazimika kuuza maembe yao kwa bei duni kabisa ili wasije wakapata hasara yatakapooza na kukosa wanunuzi.Ili kujikinga kutokana na hasara hii, Maingi Mwasaa ambaye ni mkulimu kutoka kijiji cha Ndataini, katika eneobunge la Kibwezi Mashariki, amebuni mbinu ya kipekee ya kuwezesha miembe yake kuzaa matunda mapema kabla ya msimu wa kawaida wa mavuno kutimu.

Mwasaa ambaye ni Mwalimu Mkuu katika Shule ya Upili ya Mirira, anatumia mbinu ya kisayansi ya kuingilia mfumo wa uzalishaji wa miembe ili iweze kutoa maua na kuzaa matunda mapema.

“Tunafanya hivi kwa kuvuruga utaratibu wa kuyapa miti hiyo maji. Kwanza tunakata matawi na kuinyima maji kwa kipindi cha mwezi mmoja. Hii inasababisha miembe kuanza kutoa maua. Baada ya maua kutokea, tunaanza tena kuipa maji machache huku tukiongeza maji kadri maua yanayoendelea kuota kwa wingi,” Bw Mwasaa anasema.

Anaongeza kuwa mbinu hiyo hutumika katika ukuzaji wa aina nyingi ya matunda katika msimu ambapo kuna uhaba sokoni.

“Mimea inaponyimwa mahitaji ya kimsingi kama maji na madini, wakati ambapo inakuwa, huwa inapunguza kasi ya kuzalisha matawi na kuotesha majani.

“Badala yake huelekeza rasilimali yake katika utengenezaji wa maua na sehemu zingine za kuzalisha. Mimea hutumia njia hii ili kuendelea kustahimili nyakati ngumu na kuendeleza uzalishaji,” anaeleza mkulima huyo ambaye alijifunza mbinu hii kutoka kwa wataalamu wa kilimo cha matunda mjini Murang’a.

Dkt Jane Ambuko ambaye ni mhadhiri wa kozi ya kilimo cha mboga na matunda (horticulture) katika Chuo Kikuu anasema kuwa mbinu hii ni bora za rahisi kutumiwa na wakulima haswa wale wa maeneo ya mashambani.

“Mbinu hii ya kuifanya miti ya matunda kuzalishaji kabla ya msimu wake wa kawaida kutimu imepata umaarufu kwa sababu haigharimu fedha nyingi na inawasaidia wakulima kupata faida kubwa. Mbinu hii inaleta ufanisi mkubwa haswa kwa wakulima wanaokumbatia kilimo cha unyunyiziaji wala sio wale wanaotegemea mvua,” Dkt Ambuka aliambia jarida la Akilimali.

Mwasaa anasema miezi minne baada ya miembe yake kuotesha maua, huzaa matunda.“Mimi huhakikisha kuwa miembe imepata maji ya kutosha baada ya maua kunyauka; ili kurahisisha kukomaa kwa matunda nay awe tayari kuvunwa. Kwa mfano katika shamba hili nilianza kuvuna maembe mnamo mwezi wa Septemba mwaka huu na tangu wakati huu nimekuwa nikiuza matunda hayo katika masoko ya humu nchini na hata nje,” akasema tulipokutana naye katika shamba lake la ukubwa wa ekari mbili na nusu.

Katika kilimo chake, Mwasaa hutumia maji kutoka mto Athi ulioko umbali wa mitaa 700 kutoka shambani mwake. Mkulima huyo anakuza miembe ya kisasa ambayo ina uwezo wa kuzalisha kati ya maembe 200 na 500 kwa kila mti.

“Wafanyabiashara kutoka sehemu mbalimbali hupiga foleni shambani mwangu wakati kama huu wa kiangazi kununua maembe. Miongoni mwao ni wale ambao hulenga kuuza zao hili katika masoko ya ng’ambo haswa mataifa ya Uarabuni kama vile Muungano wa Milki ya Kiarabu (UAE),” asema mwalimu huyu ambaye alianza kilimo cha maembe miaka mitatu iliyopita.

“Wao hununa matunda makubwa kwa Sh30 kila moja huku yale ya saizi ya kadri wakinunua kwa Sh20 huku wakilipa Sh10 kwa matunda madogo,” Mwasaa anaeleza.

Hii ni tofauti kabisa na bei ya maembe katika kaunti ya Makueni msimu wa mavuno ambapo matunda huuzwa kwa Sh10 kwa kilo moja huku baadhi ya wakulima wakipata hasara baada ya matunda yao kuharibika shambani.

“Japo serikali ya kaunti imetusaidia kuanzisha kiwanda cha kutengeneza juisi ya maembe, sio wote huweza kupata nafasi ya kuwasilisha maembe yao kiwandani hicho cha Kalamba Friut Processor. Baadhi wanalazimika kupeleka maembe yao sokoni ambako bei ni duni,” aeleza afisa wa kaunti ambaye aliomba tulibane jina lake.

Afisa huyo alisifia mbinu ambayo mkulima Mwasaa amekumbatia kupata faida kutokana na kilimo chake cha maembe akisema ni mfano bora wa kuigwa na wakulima haswa wale ambao mashamba yao yako karibu na mito.