Habari

Aladwa aunga mkono pendekezo la Ruto kusaidia kusimamia Kaunti ya Nairobi

Na KEVIN CHERUIYOT October 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MBUNGE wa Makadara, George Aladwa, amesema anaunga mkono uamuzi wa Rais William Ruto wa kusaidia katika usimamizi wa Kaunti ya Nairobi akisema itasaidia kumaliza changamoto za sasa.

Bw Aladwa ambaye alihudumu kama Meya wa Nairobi enzi za serikali za mitaa, alisema jiji la Nairobi ni sehemu ya utawala ambayo inastahili kuvaliwa njuga na serikali ya kitaifa na ile ya kaunti.

“Naunga mkono tangazo la Rais kwa Nairobi kwa sababu ili kuwavutia wawekezaji na ustawi wa maendeleo, Nairobi lazima iwe safi. Pia lazima kuwe na mpangilio unaoeleweka wa jinsi masuala mbalimbali yanavyoendeshwa jijini,” akasema Bw Aladwa.

Akiongea na Taifa Leo, Bw Aladwa aliwataka viongozi wa Kaunti ya Nairobi kushughulikia changamoto tele ambazo zinawaathiri wakazi wa jiji.

Alitaja takataka ambazo hazijazolewa na msongamano wa magari kama baadhi ya changamoto ambazo zinastahili kupata utatuzi.

Pia mbunge huyo anayehudumu muhula wa pili alisema hatua ya serikali kuu kuingilia usimamizi wa shughuli za Nairobi inaonyesha kuwa utendakazi wa Gavana Johnson Sakaja haujaridhisha.

“Hii ina maana kuwa kuna kitu ambacho si sawa katika kaunti hii. Inaibua wasiwasi kuwa utendakazi wa Gavana Sakaja hauridhishi hata uongozi wa nchi,” akaongeza Bw Aladwa.

Mbunge huyo ambaye pia ni mwenyekiti wa ODM Kaunti ya Nairobi alikuwa mstari wa mbele kumwokoa Bw Sakaja wakati ambapo madiwani wa Kaunti ya Nairobi walikuwa wamepanga kumbandua madarakani miezi miwili iliyopita.

Bw Aladwa, Rais William Ruto, Kinara wa upinzani Raila Odinga na aliyekuwa waziri Fred Gumo waliandaa vikao na madiwani hao ambao walishawishiwa wampe Bw Sakaja muda ili aimarishe uongozi wake jijini.

Alikiri kuwa walikubali gavana apewe miezi miwili kushughulikia baadhi ya changamoto ambazo madiwani walikuwa wamelalamikia.

Kati ya changamoto hizo mfumo wa duni wa ukusanyaji wa takataka na kucheleweshwa kwa kusambazwa kwa basari.