Aliyekiri mauaji ya wakili alivyofichua eneo la tukio
Na RICHARD MUNGUTI
MSHUKIWA wa mauaji Peter Ngugi Kamau aliyepewa Sh2,000 kumwandama wakili Willie Kimani, mteja wake na dereva wa teksi kabla ya kuuawa kwao kinyama na maafisa wa polisi wa utawala, aliwapeleka maafisa wa uchunguzi eneo la mauaji na mtoni walikotupa miili yao.
Akitoa ushahidi mbele ya Jaji Jessie Lesiit, afisa wa polisi Joseph Muindi alisema Kamau, ambaye ameshtakiwa pamoja na waliokuwa polisi wa utawala Inspekta Fredrick Leliman, Stephen Cheburet Morogo, Sylvia Wanjiku na Sajini Leonard Maina Mwangi, aliwaongoza maafisa wa polisi kuchukua picha za video mnamo Agosti 10, 2016.
“Kamau aliletwa katika afisi yangu na Inspekta Clement Mwangi anayechunguza kesi hii ya mauaji na kuniomba niwasaidie kuchukua video za pahala walipouliwa Kimani, Josphat Mwenda na Joseph Muiruri mnamo Juni 23, 2016,” Bw Muindi alimweleza Jaji Lesiit.
Alisema kabla ya kuwapeleka pahala tofauti tofauti, alimweleza Kamau kuwa anakabiliwa na shtaka la kuwaua Kimani, Mwenda na Muiruri.
Baada ya kumweleza hayo alimsomea shtaka na kumchukua video akiwa katika afisi yake.
“Tulitoka katika afisi yangu katika makao makuu ya uchunguzi wa jinani (DCI) na kufululiza hadi kwenye seli alikowafungia wahasiriwa hao watatu katika kituo cha polisi cha utawala cha Mlolongo,” alisema Bw Muindi.
Afisa huyo wa polisi mwenye cheo cha naibu wa Suparitenda alisema kutoka hapo walienda kuchukua video za Mahakama ya Mavoko na eneo walipowateka nyara katika kivuko cha garimoshi kwenye reli mjini Athi River, Kaunti ya Machakos.
“Kutoka Mavoko tulienda eneo la mauaji kando ya barabara kuu ya Nairobi-Mombasa. Kutoka pale tukaenda Kwambira iliyoko Limuru alipoacha gari la teksi la Bw Muiruri na hatimaye akatupeleka Donyo Sabuk ambapo walitupa miili ya watatu hao katika mto Athi River,” Jaji Lesiit alielezwa.
Afisa huyo wa polisi ambaye ni mtaalam wa kuunganisha ushahidi kwa njia ya picha alisema “niliombwa tu kuchukua picha za video ndipo ushahidi wa mauaji ya Kimani, Mwenda na Muiruri ukamilike.”
Alitengeneza video ambayo itachezwa mahakamani.
“Je Kamau aliwapeleka katika maeneo hayo kwa hiari ama alishurutishwa,” kiongozi wa mashtaka Nicholas Mutuku alimuuliza Bw Muindi.
Muindi alijibu.
“Alitupeleka kwa hiari na kutuonyesha kila walikowapeleka wahanga kabla ya kuwaua kinyama baada ya kuwatesa,” alisema Bw Muindi.
Maafisa hao wanne wa polisi na Kachero Kamau wamekana mashtaka ya kuwaua kinyama Kimani, Mwenda na Muiruri usiku wa Juni 23/24, 2016 katika eneo la Mlolongo.
Kesi inaendelea.
Akitoa ushahidi mbele ya Jaji Jessie Lesiit, afisa wa polisi Joseph Muindi alisema Kamau anayeshtakiwa pamoja na waliokuwa polisi wa utawala Inspekta Fredrick Leliman, Stephen Cheburet, Sylvia Wanjiku na Sajini Leonard Maina Mwangi aliwaongoza maafisa wa polisi kuchukua picha za video mnamo Agosti 10, 2016.