Aliyekuwa mwenyekiti TLB afariki kutokana na kansa
Na GEORGE SAYAGIE
ALIYEKUWA mwenyekiti wa Bodi ya Utoaji Leseni katika Sekta ya Uchukuzi (TLB), Hassan Ole Kamwaro amefariki kutokana na kansa katika hospitali moja nchini Amerika.
Chanzo cha familia yake kimesema Kamwaro alikuwa katika Mercy Hospital, Oklahoma, Amerika.
Familia hiyo ikihutubia wanahabari Jumatano nyumbani Eor-Enkitok, kaunti ndogo ya Narok Kaskazini, msemaji wake Martin Ole Kamwaro amesema walipata tanzia Jumanne jioni.
“Tulipokea tanzia kuhusu kifo cha kakangu jana (Jumanne) jioni. Madaktari walitueleza kwamba alizirai kabla ya kufikishwa katika chumba cha wagonjwa mahututi. Walitueleza kwamba alifariki dakika chache baadaye kwa sababu ubongo ulikosa kufanya kazi kwani damu ilikosa kuufikia,” amesema Bw Kamwaro.
Marehemu Kamwaro aliteuliwa tena mwenyekiti wa TLB Desemba 2010 na Rais (Mstaafu) Mwai Kibaki.
Ni kipindi hicho ambapo magari ya uchukuzi wa umma yaliwekwa vidhibiti kasi na mikanda ya kuhakikisha usalama licha ya pingamizi kutoka kwa wadau.
Mkewe, Regina Kamwaro, aliangamia katika ajali barabarani na miaka michache baadaye akaoa mke wa pili – Bi Judith Kamwaro – ambaye vyanzo vinasema alimuacha kwenye mataa wakati akiugua.
Desemba 2013 akiwa na umri wa miaka 69, Kamwaro alioa tena; mara hii mke wa tatu, Bi Eunice Sossion aliyekuwa na umri wa miaka 23 katika sherehe ya kitamaduni ya jamii ya Maasai
Marehemu Ole Kamwaro ameacha watoto 20 na wajukuu kadhaa.