Habari

Aliyekuwa Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe afariki

September 6th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MWANGI MUIRURI

ALIYEKUWA Waziri Mkuu na hatimaye Rais wa taifa huru la Zimbabwe, Robert Mugabe ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 95.

Kwa wengine, bila kuzingatia hisia za ubaguzi wa rangi, mwendazake atabakia katika kumbukumbu za mashujaa wa kutetea haki za ngozi nyeusi, lakini kwa wengine akibakia kuwa nembo ya utawala wa kiimla katika taifa lake.

Aliongoza baina ya 1980 hadi 2017 alipotimuliwa na jeshi la taifa hilo na Emmerson “Mamba” Mnangagwa akachukua hatamu za urais.

Ifahamike kwamba alianza katika wadhifa wa Waziri Mkuu. Rais wa kwanza mweusi Zimbabwe alikuwa ni Canaan Sodindo Banana.

Banana ambaye alikuwa mwanasiasa na Msomi wa Maswala ya Dini, ndiye Rais wa kwanza Mwafrika Zimbabwe, ambaye pamoja na Mugabe na Mnangagwa walipigania uhuru wa nchi hiyo kutoka kwa serikali ya Mkoloni. Aidha, Zimbabwe ilipata uhuru 1980. Sodindo Banana alizaliwa Machi 5, 1936, Esigodini, Southern Rhodesia kama ilivyojulikana Zimbabwe chini ya utawala wa Wabeberu. Alisomea shule ya msingi ya Kimishonari ya Mzinyati, kisha akajiunga na ya sekondari ya Tegwani. Baadaye alisomea taaluma ya ualimu kabla ya kujiunga na taasisi ya mafunzo ya Dini ya Epworth, Harare.

Ripoti zilizotiwa rasmi na familia na serikali Zimbabwe zimesema kuwa Mugabe aliaga dunia Alhamisi akipokezwa matibabu katika taifa la Singapore.

Mwaka wa 2017 aking’atuliwa mamlakani kupitia shinikizo za ajiuzulu alipewa chaguo la kuhamishwa hadi nje ya nchi na akwepe kushtakiwa kwa madai ya udhalimu wa kiutawala lakini akajibu: “Mimi mzalendo kamili kwa Taifa langu naomba nikubaliwe niishi papa hapa Zimbabwe na ikiwa nitaaga dunia, iwe ni katika udongo ulio katika mipaka ya taifa hili langu.”

Tutakuletea baadaye mengi kuhusu maisha ya mwendazake kupitia makala za kina.

Na kwa kuwa mauti ni maamuzi ya Maulana aliye mumiliki wa uhai, Mugabe aliyehudhuria hafla rasmi ya uzinduzi wa Katiba Mpya ya Kenya mwaka wa 2010, hana lingine ila tu kutii mwito na kumenyana na hukumu mbele ya haki, walio hai wakiwa lao tu ni kumpungia mkono wa buriani.