Habari

Aliyeshukiwa kuua mpenzi adaiwa kujinyonga akiwa seli

Na VITALIS KIMUTAI January 17th, 2026 Kusoma ni dakika: 1

MSIBA mara mbili umekumba Kaunti ya Bomet baada ya mwanaume anayehusishwa na mauaji ya mpenzi wake mjamzito kufariki kwa madai ya kujitoa uhai akiwa mikononi mwa polisi.

Familia ya Caroline Chepkoech Ngetich, mwalimu wa Shule ya Sekondari Msingi ya Cheptagum katika Kaunti Ndogo ya Bomet Mashariki, ilikuwa ikiendelea na maandalizi ya mazishi yake pale ilipopata habari kwamba mshukiwa mkuu wa mauaji yake naye alikuwa amefariki.

Caroline, mwenye umri wa miaka 33, aliajiriwa hivi majuzi na Tume ya Huduma ya Walimu (TSC). Alifariki Januari 5, 2026, katika mazingira ya kutatanisha.

Mshukiwa, Anthony Njenga Kariuki, pia mwenye umri wa miaka 33, anaripotiwa kujitoa uhai Alhamisi jioni kwa kutumia soksi alipokuwa akizuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Longisa, Kaunti Ndogo ya Bomet Mashariki.

Vifo vya wawili hao, waliokuwa wakiishi pamoja katika Kituo cha Biashara cha Longisa, vimeacha maswali mengi kuliko majibu.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Bomet Mashariki, Michael Mwenda, alisema mshukiwa alikamatwa siku tatu kabla ya kifo chake baada ya ripoti ya upasuaji wa maiti kutofautiana na maelezo aliyotoa kuhusu kifo cha mpenzi wake.

“Mshukiwa alikamatwa na kufikishwa mahakamani Alhamisi mchana, ambapo mahakama iliamuru azuiliwe kwa siku saba akisubiri uchunguzi kabla ya kusomewa mashtaka,” alisema Bw Mwenda.

Aliongeza kuwa baadaye jioni, afisa wa polisi aliyekuwa akifanya ukaguzi wa kawaida alipata mshukiwa amejitoa uhai selini.

Mwili wake ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Longisa, ambako pia mwiliwa Caroline ulikuwa umehifadhiwa ukisubiri kuchukuliwa na jamaa mazishi yaliyopangwa kufanyika Ijumaa.