Aliyesimamia ofisi ya Ruto ‘amvua nguo’ seneta mahakamani
Na SAM KIPLAGAT
KESI ya talaka kati ya Seneta wa Meru Mithika Linturi na Aliyekuwa Msimamizi Mkuu katika Afisi ya Naibu Rais William Ruto, Bi Marianne Kitany iliendelea kortini Jumatano, afisa huyo akifichua namna alivyopata utajiri wanaozozania bila usaidizi wa mwanasiasa huyo.
Bi Kitany alianza kwa kusimulia mahakama jinsi Bw Linturi alivyotembelea nyumbani kwa wazazi wake Kaunti ya Nandi na akalipa mahari.
Alimweleza Hakimu Mkuu wa Milimani, Peter Gitonga kwamba Bw Linturi aliongoza ujumbe wa watu 19 kutoka Igembe, Meru kutimiza hitaji hilo la kitamaduni, ishara kwamba walikuwa wameoana rasmi.
Kulingana naye, Seneta huyo ambaye wakati huo alikuwa mbunge wa Igembe Kusini alimlipia mahari ya Sh100,000 kisha akampa zawadi mamake gari la aina ya Nissan X-Trail.
“Aliambia mamangu kwamba awe akitumia gari hilo kununua bidhaa, kuteka maji mtoni na majukumu mengine ya nyumbani. Hii ni kwa sababu msichana wake hangewajibikia majukumu hayo tena baada ya kuolewa,” akasema Bi Kitany.
Alipoulizwa na wakili wake Danstone Omari nani aliongoza ujumbe ulioandamana na Bw Linturi kwenye hafla hiyo, Bi Kitany alifichua kuwa Bw Rufus Miriti na mkewe ndio walikuwa mstari wa mbele katika sherehe hiyo.
Bi Kitany pia alisimulia namna Bw Linturi alivyohamia nyumba yake ya kifahari baada ya kushindwa kumudu kodi ya Sh200,000 ya nyumba aliyokodisha katika barabara ya Ngong. Alifichua kwamba wakati moja alimsaidia na kiasi hicho cha fedha baada ya kulemewa na kodi.
Isitoshe, alifunguka na kusema aligharimia fungate yao katika mataifa ya Australia, Mauritius na Dubai kando na kutoa fedha wakati walipoandamana na watoto wao kwenda kujivinjari Zanzibar.
Kumtambulisha kwa wanasiasa
Vilevile Bi Kitany alieleza korti kuwa Bw Linturi alimjulisha kama mke wake kwa wanasiasa wenzake akiwemo Gavana wa Meru Kiraitu Murungi.
Wakati wa kikao cha mahakama, Bi Kitany pia alifichua kwamba aliwajengea wakwe zake makazi ya kifahari yaliyomgarimu Sh8 milioni.
Bi Kitany aliwasilisha kesi hiyo ya talaka akimlaumu seneta huyo kwa ukali, kumtelekeza, kutokuwa mwaminifu katika ndoa na kumnyima tendo la ndoa.
Wawili hao walikuwa wakiishi pamoja kwenye makazi yao mtaani Runda hadi mwezi Septemba 2018 wakati Bw Linturi alipomfurusha.
Hata hivyo, Bi Kitany alielekea kortini na kupata amri ya kuendelea kuishi kwenye makazi hayo hadi kesi ya talaka aliyowasilisha isikizwe na kuamuliwa.
Kesi ya wawili hao itaendelea August 28.