Amerika yapitisha kura kumng'oa Trump mamlakani
NA AFP
WASHINGTON, Amerika
BUNGE la Congress nchini Amerika Jumatano lilipitisha kura ya kumwondoa mamlakani Rais Donald Trump kwa kutumia vibaya mamlaka ya afisi yake na kuingilia uchunguzi wa bunge hilo, hatua ambayo imetoa nafasi kwa bunge la Seneti kuamua ikiwa atasalia mamlakani au la.
Hatua hiyo sasa inamfanya Bw Trump, 73, kuwa rais wa tatu katika historia ya Amerika kuwahi kukataliwa na bunge hilo la wawakilishi. Wengine ambao wamewahi kukataliwa ni wabunge ni; Andrew Johnson mnamo 1868 na Bill Clinton (1998) lakini waliponea kwani seneti ilidinda kuwaondoa mamlakani.
Katika kosa la kwanza, wabunge 230 wa bunge hilo la wawakilishi walipiga kura ya kumwondoa huku 197 wakipinga. Na kwa kosa la pili wabunge 229 walipiga kura ya kumng’oa huku 198 wakipiga kura ya kupinga katika hoja hiyo iliyowasilishwa na mbunge wa chama kikuu cha upinzani, Democrats, Adam Schiff.
Schiff anadai kuwa Trump alimtumia mamlaka ya afisi yake kumshinikiza rais mpya wa Ukraine Volodymyr Zelenkyy amchunguze mpinzani wake mkuu katika uchaguzi ujao wa urais Joe Bidens kuhusiana na sakata ya ufisadi iliyotokea humo.
Mwanawe Bidens, ambaye alikuwa makamu wa rais chini ya utawala uliopita wa Barak Obama aliwahi kuhudumu katika kampuni moja ya gesi nchini Ukraine na ambayo ilihusishwa na sakata hiyo.
Ilidaiwa kuwa Trump alitaka kutumia habari kuhusi sakata hiyo kumchafulia jina Bw Biden ambaye anapigiwa upatu kuteuliwa kama mgombea urais wa chama cha Democrat katika uchaguzi mkuu wa Novemba 16, 2020.
Katika kosa la pili, wabunge wa Democrat wanamlaumu Bw Trump kwa kumtumia mamlaka yake kujaribu kuzuia bunge la Congress kuchunguza njama zake na Ukraine.
Lakini licha ya bunge la Congress kupitisha hoja ya kutaka kumwondoa Trump mamlakani huenda hatua hiyo ikabatilishwa na Seneti ambako Trump ana idadi kubwa ya wanachama wa Republican.
Imetafsiriwa na Charles Wasonga