Habari

Askari jela aliyedaiwa kushiriki maandamano afikishwa kortini

Na RICHARD MUNGUTI January 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

ASKARI wa magereza aliyedaiwa kushiriki maandamano ya kupinga serikali mnamo Juni 2024 Alhamisi alifikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuchochea uasi na kuchapisha taarifa za uongo katika mtandao wa X akaunti ya Shakur The Cop @CopShakur.

Bw Jackson Kuria Kihara, alikamatwa siku chache baada ya Waziri wa Masuala ya Ndani Kipchumba Murkomen kuonya kwamba, wale wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii watakabiliwa na ghadhabu na nguvu kamili za sheria.

Bw Kihara aliwasilishwa mbele ya Hakimu Mkuu wa Milimani Lucas Onyina na upande wa mashtaka ukaomba polisi waruhusiwe kumzuilia kwa siku 21 ili kuwezesha maafisa wa Upelelezi wa Jinai (DCI) kumchunguza zaidi.

“Maafisa wa DCI wanamchunguza Kihara kwa makosa ya kuchochea uasi na kuchapisha habari za uongo kinyume cha Kifungu cha 23 cha Sheria ya Matumizi mabaya ya Kompyuta na uhalifu wa mtandao,” kiongozi wa mashtaka aliambia korti.