Habari

Askofu Mwai alazimika kutupa laini ya simu sababu ya ‘salamu za Gen Z’

Na SIMON CIURI March 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

ASKOFU Mkuu wa Kanisa la Jesus Winners Ministry, lililoko Roysambu, Nairobi, Edward Mwai, amelazimika kutupa laini yake ya simu ambayo amekuwa nayo kwa zaidi ya miaka 15 baada ya ‘kupokea salamu’ kutoka kwa Wakenya waliojawa na hasira.

Hii ni baada ya askofu huyo kupigiwa simu na kupokea jumbe zisizo na kikomo kutoka kwa vijana waliojawa na hasira wakitaka majibu kuhusu mchango wa Sh20 milioni uliotolewa na Rais William Ruto.

”Nimepokea zaidi ya jumbe 5, 000 za matusi na siwezi kupiga simu. Sawa na mke wangu. Kwa sasa tunapanga kubadilisha nambari zetu za simu,’’ Bw Mwai alisema katika mahojiano na Taifa Dijitali.

”Rais Ruto hakuziacha pesa hizo mikononi mwangu baada ya kutoa tangaza hilo mbele ya waumini. Kila kitu kilikuwa kikirekodiwa na hakuna mahali mimi au mtu yeyote kutoka kanisani alipokea mchango huo kutoka kwa rais. Binafsi sipokei sadaka moja kwa moja wala sihesabu, kuna watu wanafanya hivyo na wameniambia hadi sasa hawajapokea chochote kutoka kwa Rais lakini tutafuatilia ahadi hiyo,” Bw Mwai aliongeza.

Msemaji wa Ikulu hata hivyo hakujibu swali letu la iwapo Rais Ruto alitoa Sh20 milioni kwa kanisa la Bw Mwai Jumapili. Mnamo Alhamisi, Rais alikutana na Askofu Mwai katika ikulu ya Nairobi baadhi ya Wakenya wakifasiri alienda kuchukua hela alizoahidiwa wikendi.

Jumbe hizo za matusi na simu zisizo na kikomo zimemfanya Bw Mwai kuingiwa na hofu na hali ya wasiwasi, hivi kwamba wakati wa mahojiano alisitasita kupigwa picha.

Bw Mwai alitaja sababu za faragha, lakini akadokeza kwamba ana wasiwasi kuhusu habari ambazo zingechapishwa  baada ya mahojiano.

”Nina wasiwasi kuhusu utakachoandika baada ya mahojiano haya. Ukiandika kisa chenye uwiano, mema ya Mola yakufuate, ukiamua kufanya vinginevyo, namwachia Mungu,’’ alisema huku akitabasamu, huku msaidizi wake akitoa kikombe cha chai.

Wakati wa ibada Jumapili, Rais Ruto aliahidi kuchanga Sh20 milioni kwa kanisa la Bw Mwai na hata kuahidi kutoa Sh100 milioni katika harambee “ambayo nitahudhuria pamoja na marafiki zangu” yote hayo kuelekea ujenzi wa kanisa jipya.

“Katika ujenzi wa kanisa letu hapa, mimi mwenyewe nitatoa Sh20 milioni kwanza,” Rais Ruto alisema huku kanisa likisherehekea kwa vigelegele.

Ahadi hiyo iliibua kero miongoni mwa Wakenya waliohoji kuhusu hatua ya Rais Ruto kuyapa kipaumbele masuala ambayo hayana manufaa ya moja kwa moja kwa Wakenya.

Kupitia jumbe kadhaa katika mitandao ya kijamii, Wakenya walitaka kujua ikiwa Rais amebatilisha marufuku aliyoweka dhidi ya watumishi wa umma kushiriki harambee baada ya maandamano ya vijana wa Gen Z mwaka jana.

Askofu huyo alisema katika maisha yake yote ya huduma, wiki hii amepitia wakati mgumu baada ya Wakenya waliojawa na hasira kusambaza nambari yake ya simu ya kibinafsi na ya mke wake kwenye mitandao ya kijamii.

IMETAFSIRIWA NA WINNIE ONYANDO