Askofu wa Siaya aliyetoweka Januari apatikana ameuawa
Na CHARLES WASONGA
MWILI wa Askofu Charles Oduor Awich aliyetoweka katika eneobunge la Alego Usonga, Kaunti ya Siaya Januari 2020 ulipatikana katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya Port Victoria.
Awich ambaye alikuwa kiongozi wa Kanisa la Roho Judea alitoweka huku kukidaiwa kuwa alitekwa nyara na watu wasiojulikana kutoka nyumbani kwake.
Jamaa zake wamekuwa wakimsaka tangu wakati huo hadi Ijumaa walipopata maiti yake.
Kulingana na Mwenyekiti wa Muungano wa Viongozi wa Makanisa, Kaunti ya Siaya Askofu Mkuu James Opiyo, mwili wa Awich ulikuwa na majeraha kadhaa ya kisu na ulitambuliwa na mkewe Helen Auma Oduor.
Opiyo aliwaambia wanahabari kwamba alipata habari kwamba mwili huo ulipelekwa na polisi katika hifadhi hiyo ya maiti baada ya kupatikana katika ufuo wa Ziwa Victoria.
Askofu huyo mkuu alikosoa jinsi polisi wa walivychunguza suala la kupotea kwa marehemu Awich.
Opiyo aliwataka polisi kuendelea na uchunguzi zaidi akisema hakuna namna wangedai kwamba walishindwa kupata habari kuhusu alikokuwa Awich mwezi mmoja baada ya kutoweka kwake.
Kamanda wa polisi katika kaunti ndogo ya Siaya, Justus Kucha alithibitisha kisa hicho lakini akasema angetoa maelezo zaidi kuhusu suala hilo.
Askofu huyo alitoweka mapema Januari huku duru zikisema kuwa alikuwa ametekwa nyara. Wakati huo, mkewe Awich aliwaambia maafisa wa polisi kwamba mumewe alihusika katika mzozo wa ardhi na baadhi ya jamaa zake.