Habari

Asukumwa jela miezi sita kwa kudai bangi inamsaidia kufanya kazi

Na GEORGE MUNENE January 17th, 2026 Kusoma ni dakika: 1

MAHAKAMA ya Wang’uru, Kaunti ya Kirinyaga, ilishtuka baada ya kijana mmoja kukiri waziwazi kuwa anavuta bangi ili aweze kuhimili kazi ngumu ya kufukuza ndege katika mashamba ya mpunga eneo la Mwea.

Brian Macharia alishtakiwa kuwa mnamo Januari 9 mwaka huu katika kijiji cha Kiriko, Kaunti ya Kirinyaga, alipatikana na misokoto tisa na nusu vya bangi ya thamani ya Sh950.

Aliposomewa shtaka, Macharia alikiri kosa hilo bila kusita na kuomba mahakama imsamehe.

“Ni kweli nilikuwa na bangi hiyo. Navuta bangi kwa sababu kazi ninayofanya ni ngumu sana. Sasa nimetambua kuwa ni kinyume cha sheria kumiliki na kuvuta bangi. Naomba mahakama inisamehe. Sitafanya kosa hilo tena,” alisema, kauli iliyowashangaza wengi waliokuwa mahakamani.

Macharia alieleza kuwa yeye ni kibarua anayejipatia riziki kwa kufukuza ndege kwenye mashamba ya mpunga, na kwamba alikuwa akitumia bangi ili aweze kufanya kazi hiyo ipasavyo.

Baada ya kusikiliza maelezo yake, Hakimu Mkuu Martha Opanga alimhukumu Macharia kulipa faini ya Sh10,000 au kutumikia kifungo cha miezi sita jela iwapo atashindwa kulipa.