Habari

Atwoli achemsha wandani wa Ruto, wataka akamatwe

October 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na ERIC MATARA

WANDANI wa Naibu Rais Dkt William Ruto kutoka Kusini mwa Bonde la Ufa, sasa wanataka Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi(COTU), Bw Francis Atwoli, akamatwe kwa kudai Naibu Rais Dkt William Ruto hatakuwa debeni mwaka wa 2022.

Viongozi hao waliowajumuisha wabunge, madiwani na Baraza la Wazee wa Bonde la Ufa, wanadai kwamba matamshi ya Bw Atwoli ni ya kichochezi na yanagawanya taifa hili.

Wanasiasa hao sasa wanataka Idara ya Upelelezi(DCI) kuchunguza tamko alilotoa Bw Atwoli Jumapili wakati wa hafla ya kuchangisha fedha katika kanisa la Kiadventista la Bukhwala, Khwisero, kwamba Dkt Ruto anapoteza wakati wake bure akifanya kampeni za uchaguzi huo ilhali hatakuwa debeni.

“Leo nataka kuwaambia kwamba Naibu Rais hatakuwa Rais 2022. Anafaa akome kupoteza wakati wake bure,” akasema Bw Atwoli.

Mbunge wa Kuresoi, Bw Joseph Tonui amevitaka vyombo vya usalama kuharakisha na kumtia mbaroni mkuu huyo wa chama cha wafanyakazi.

“Ni jambo la wazi kwamba matamshi ya Bw Atwoli ni ya chuki na anaeneza ukabila kuelekea uchaguzi wa 2022. Hii ni hali hatari na anafaa kukamatwa kisha afikishwe mahakamani kwa kutoa matamshi ya uchochezi. Yeye ni shida kwa taifa hili,” akasema Bw Tonui.

Kauli yake iliungwa mkono na mbunge wa Molo, Bw Kuria Kimani ambaye alisema mtu wa hadhi ya Bw Atwoli hafai kutoa matamshi mabaya dhidi ya Naibu Rais.

“Haya ni matamshi ambayo hayafai kutoka kwa mtu ambaye ni mzee. Hafai kuruhusiwa kundelea kutoa matamshi hayo yasiyofaa,” akasema Bw Kimani.

“Huyu jamaa hana ajenda zozote kwa taifa hili na Wakenya wanafaa kumpuuza,” akasema Mbunge wa Belgut, Bw Nelson Koech.

Wabunge wengine kutoka ngome ya Dkt Ruto ambao walizungumza na Taifa Leo pia walishutumu matamshi ya Bw Atwoli na kutaka serikali imchukulie hatua kali.

“Bw Atwoli anafaa atueleze alichomaanisha kwa kusema Naibu Rais hatakuwa Rais. Kama viongozi kutoka Bonde la Ufa tunamshuku sana. Anafaa kuonywa dhidi ya kutoa matamshi kama hayo wakati Rais Uhuru Kenyatta anaendelea kuhubiri umoja miongoni wa raia wa nchi yote,” akasema mbunge mmoja kutoka Kaunti ya Nakuru aliyeomba jina lake lisitajwe.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee kutoka Bonde la Ufa, Bw Gilbert Kabage naye aliwaongoza wazee wenzake kumtaka Bw Atwoli aombe msamaha kutokana na kauli alizotoa dhidi ya Dkt Ruto.

“Tumempa Bw Atwoli siku saba kuomba msamaha kwa Naibu Rais na Wakenya. Hatutamruhusu apandishe joto la kisiasa kuhusu urithi wa kiti cha Urais 2022,” akasema Bw Kabage.

Diwani wa Lake View, Bw Karanja Mburu naye aliwaongoza madiwani 20 kukemea matamshi ya Bw Atwoli.