Habari

Atwoli awafokea wanaomshinikiza Rais ahudhurie mikutano ya BBI

March 6th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na BRENDA AWUOR

KATIBU Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi nchini (Cotu-K) Bw Francis Atwoli, ameonya wanasiasa wanaosikika mara kwa mara wakishinikiza Rais Uhuru Kenyatta kuhudhuria mkutano wa uhamasisho wa Mpango wa Maridhiano (BBI) unaotarajiwa kufanyika Nakuru.

Bw Atwoli, ameonya wafuasi wa Naibu Rais William Ruto, ambao wamekuwa ‘wakimlazimisha’ Rais Uhuru Kenyatta kuhudhuria mkutano wa BBI unaopangwa kufanyika Nakuru, Machi 21.

Pia ameonya na kusema kwamba hakuna yeyote atafanikiwa kuzuia au kuzima mikutano ya BBI.

“Rais ana uwezo wa kujiamulia cha kufanya ila si kulazimishwa na baadhi ya viongozi ndani ya Jubilee,” amesema Atwoli akiongeza “tuna uwezo wa kugharimia mahitaji ya BBI.”

Amesema haya akihutubu katika mkutano ulioandaliwa katika Chuo cha Mafunzo ya Leba cha Tom Mboya ambapo alikutana pia na wakuu wa Bima ya Afya ya Kitaifa (NHIF).

Hii ni baada ya wafuasi wa Ruto, wakiongozwa na naibu katibu mkuu wa chama cha Jubilee Bw Caleb Kositany, kutaka Rais kuhudhuria mkutano wa BBI Nakuru.

Wamemtaka Rais kuhudhuria mkutano wa BBI; zao la handisheki baina ya Rais na Kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kama njia ya kukuza umoja miongoni mwa Wakenya.

Bw Atwoli amependekeza wakuu wa NHIF kuteua kamati ambayo itakuwa inatetea wafanyakazi wa nchi kutokana na changamoto wanazopitia huku akionya wanahabari wanaotangaza hali ya shirika la NHIF kuzorota akisema upo wakati ambapo aghalabu kila sekta hukumbwa na changamoto.

Kiongozi huyo ni mwanachama wa bodi ya wadhamini katika NHIF.

Amesema asilia 99 ya wafanyakazi ni wezi ndiposa kampuni zinakumbwa na changamoto kifedha na kutaka NHIF kuanza kuchunguza atakayemfuata kwa lengo la kurithi nafasi akitoka ofisini; mtu ambaye atahakikisha kukua kwa shirika.

“Wafanyakazi asilimia 99 ni wezi, naomba wakuu wa NHIF kuanza kuchunguza atakayefaa nitakapoondoka ofisini,’’ amehitimisha.

Wakuu wa NHIF wakiongozwa na Bw Nichodemus Odongo, wamepinga juhudi zozote za Mamlaka ya Kudhibiti Bima (IRA) kusimamia fedha za NHIF kwa kukosa imani na shirika hilo.

‘’Tunapinga juhudi zozote za IRA kusimamia fedha za NHIF kwa sababu itaendelea na shughuli zake kama kawaida na tunatarajia manufaa kwa wafanyakazi,’’ Bw Odongo amesema.