Habari

Atwoli: Tusipofanya jambo chuki mitandaoni itachoma nchi

Na KEVIN CHERUIYOT April 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KATIBU Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi nchini Francis Atwoli amekosoa vijana kwa kumwaga hasira zao mitandaoni na akawataka wabadilishe mtazamo wao dhdi ya viongozi.

Akizungumza katika kanisa la ACK St Stephen’s, Makadara, Jumapili, Bw Atwoli alisema mitandao itachoma nchi isipodhibitiwa.

“Hii kitu inaitwa social media imedhibitiwa Uchina. Tiktok imedhibitiwa huko licha ya kuwa ni mtandao wao waliounda, sio kama hapa Kenya. Kanisa lapaswa kuzungumza kuhusu Tiktok, kanisa lazima liongee kuhusu social media na kuhusu YouTube. Kanisa lazima litoe muongozo,” akasema.

Alisema kwamba yaliyomo kwenye mitandao “si yafaayo kwa taifa linalotaka kufikia viwango vya juu kiuchumi, kijamii na kisiasa.”

Alidai kwamba wengi wa vijana kwenye mitandao hawajawahi kuwa wanachama wa vyama vyovyote vya wafanyakazi nchini ilhali ndio wanaongoza kuchochea Wakenya kuchukia viongozi wao.

“Vijana walioko kwenye mitandao hawajawahi kufanya kazi kokote. Hawajawahi kuwa wanachama wa vyama vya wafanyakazi. Lakini utawaona mstari wa mbele wakizungumzia kuhusu ubaguzi kazini. Ikiwa serikali na sisi viongozi hatutafanya jambo, kutaharibika,” akasema.

Wakati huo huo, Bw Atwoli alisema kuna haja ya kudhibi habari ambazo zinawafikia vijana.

“Kila nchi hupitia kipindi cha kujiumba upya. Kenya nusura ijipate katika hali hiyo 2007 lakini Mungu akatunusuru. Hivi majuzi, kwa sababu ya maandamano ya Gen Z, tulikuwa tuone uumbaji mwingine lakini Mungu akatuokoa. Sidhani kama Mungu atatuokoa tena kwenye jaribio la tatu.”

Hata hivyo, aliwataka viongozi kuepuka siasa za kubaguana na kwamba wasaidie kusimamisha nchi kiuchumi ambao alisema ni tatizo la dunia kote.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Katibu wa Wizara ya Leba Shadrack Mwadime ambaye alimwakilisha Waziri wa Leba Dkt Afred Mutua.

Mbunge wa Makadara George Aladwa alikuwepo ila alizuiwa kuongea kufuatia amri ya kanisa hilo kutowapa kipaza sauti viongozi wa kisiasa katika ibada za Jumapili.