Habari

Atwoli: Wakenya sasa wananyimwa vibali vya kazi Tanzania sababu ya ‘vituko’ vya Karua

Na KEVIN CHERUIYOT May 27th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KATIBU Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Nchini (COTU) Francis Atwoli amedai kuwa Wakenya sasa wananyimwa vibali vya kufanya kazi Tanzania baada ya kutimuliwa kwa wanaharakati wiki jana.

Hii ni baada ya wanaharakati kutoka Kenya kufika Tanzania wakati wa kusikizwa kwa kesi ya Kiongozi wa Upinzani Tundu Lissu wiki jana lakini wakafurushwa.

Kati ya waliotimuliwa ni Kiongozi wa PLP Martha Karua, Jaji Mkuu wa zamani Willy Mutunga na mwanaharakati wa haki za kibinadamu Boniface Mwangi.

“Kutokana na uanaharakati wa Wakenya Afrika Mashariki, sasa Wakenya ambao wanafanya kazi Tanzania wananyimwa vibali. Hii inaonyesha kuwa kuna tatizo kubwa sana Afrika Mashariki,” akasema Bw Atwoli kwenye mahojiano na runinga ya NTV.

Wengine ambao walitimuliwa mwanachama wa Baraza Kuu la Chama cha Wanasheria Gloria Kimani na wanaharakati Lynn Ngugi na Hussein Khalid.

Kwa mujibu wa Bw Atwoli, wanaharakati Wakenya pamoja na viongozi wengine wanastahili kutumia diplomasia na mazungumzo iwapo kuna masuala tata ya uongozi ndipo wasiwaumize watu wengine wanaosaka ajira,

“Kama tuna shida na serikali ya Tanzania mbona wanaharakati wetu wasipitia wizara ya masuala ya kigeni badala ya kuvuka mpaka na kupeleka uanaharakati wao katika taifa huru?”

Alisema Tanzania ni taifa huru lenye sheria zake ambazo zinastahili kuheshimiwa na yeyote anayeingia nchini humo. Alisema uwepo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) haina maana kuwa uanaharakati unastahili kupelekwa katika taifa lolote lile.

“Nawaomba wanasiasa wetu wamshauri Martha Karua na wanaharakati wengine watumie wizara ya masuala ya kigeni iwapo wana tatizo na serikali za Tanzania, Uganda, Rwanda au nchi yeyote Afrika Mashariki. Hii itawaepushia hasara Wakenya wanaofanya kazi katika mataifa hayo,” akaongeza Bw Atwoli.

“Iwapo serikali hizo zitawanyima vibali kutokana na maasi na uanaharakati wetu, basi watatatizika ilhali hapa nchini hakuna ajira,”

Katibu huyo aliwataka wanaharakati hao waelekee mataifa yaliyosambaratishwa na vita kama Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) au Sudan Kusini iwapo uanaharakati wao ni wa kusaka uongozi bora.

Aliwaonya wanaharakati Wakenya kwamba kinyume na hapa nchini ambapo maisha yao yanathaminiwa, katika nchi nyingine watakabiliwa vikali na hata kuuawa ishara kuwa wanahatarisha maisha yao.