Babu mwizi asukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela
BABU wa miaka 70 aliyepatikana na hatia ya kumwibia mjane fidia ya mumewe Sh752,000 miaka 12 iliyopita atakula maharage gerezani kwa kipindi cha miezi 12 akishindwa kulipa faini ya Sh200,000 aliyotozwa mnamo Jumatatu Agosti 11, 2025.
Babu Ibrahim Kenyoru Bwana alisukumiwa kifungo hicho na hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Benmark Ekhubi.
“Hii mahakama ilikupata na hatia ya kumwibia mjane. Umehukumiwa kutumikia kifungo cha mwaka mmoja gerezani endapo utashindwa kulipa faini ya Sh200,000,” Ekhubi alimweleza Babu huyo mwizi.
Mahakama ilimpata Kenyoru na hatia ya kumwibia Hellen Kemuma Matura Sh752,526 kati ya Machi 20, 2013 na Aprili 22, 2016.
Ekhubi alisema upande wa mashtaka ulithibitisha kabisa Kenyoru akishirikiana na watu wengine kuiba pensheni hiyo ya marehemu mumewe.
Akiomba Kenyoru aadhibiwe vikali, kiongozi wa mashtaka Sonia Njoki alisema, “Mjane Kemuma na watoto wake wanaishi maisha ya uchochole kutokana kitendo cha Kenyoru.”
Akaendelea Njoki, “Pesa hizi za pensheni ya mumewe Kemuma ndizo alitazamia kuwaelimisha watoto na kujikimu kimaisha. Lakini sasa walisukumwa kwa lindi la umaskini na hata hawawezi kujikimu kimaisha. Mjane huyu na mayatima wake wanaishi maisha ya ufukara. Mwadhibu Kenyoru ipasavyo.”
Kusikia mawasilisho ya upande wa mashtaka, Kenyoru alimlilia hakimu akimsihi asimsukume gerezani kutokana nsa umri wake mkubwa.
Akamrai hakimu kwa masikitiko “Umri wangu Mheshimiwa ni zaidi ya miaka 70. Najuta nilishawishika kumwibia mjane. Naomba mahakama ipitishe adhabu badala. Aidha uniadhibu nilipe faini ama kifungo cha nje.”
Hakimu alisema atamwadhibu Kenyoru Agosti 11, 2025 baada ya kutathmini ripoti ya afisa wa urekebishaji tabia.
Pia alisema atazigatia malilio ya kikongwe huyo.
Kenyoru alishtakiwsa kuiba pesa hizo kutoka idara ya kushughulikia malipo ya pensheni ya watumishi wa umma katika jengo la Bima House iliyoko barabara ya harambee kaunti ya Nairobi.
Babu mwizi aliomba mahakama imkubalie atumie dhamana ya Sh200,000 kulipia faini.
Ekhubi alimpa siku 14 kukataa rufaa kama hakuridhika na adhabu hiyo.