Babu Owino: Hata Ruto aniweke kamba shingoni sitamuunga; akileta elimu bila malipo tutaongea
MBUNGE wa Embakasi Mashariki Babu Owino amesema yuko tayari kumuunga mkono Rais William Ruto endapo ataweka sera bora za kuimarisha sekta ya elimu.
Bw Owino ambaye amekuwa mkosoaji mkubwa wa Rais Ruto alisema anashangaa namna mwanasiasa huyo alivyobadilika tangu aingie mamlakani licha ya kutangaza alivyolelewa maisha ya uchochole.
Akiongea kwenye hafla ya elimu huko Malindi, mbunge huyo alisema yuko tayari kushirikiana na Rais endapo ataweka elimu iwe bure.
Alimpa changamoto Rais kuweka elimu ya bure kwanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu ili kuwapunguzia Wakenya gharama ya maisha ikiwemo ulipaji karo.
“Ulipochaguliwa nilijua kuwa utawatumika Wakenya vizuri sababu ya kule ulikotoka. Ulilelewa kwa biashara ya kuku na mayai, mbona umebadilika? Unataka nikuunge mkono hata uchukue kamba uniweke kwa shingo haina shida, sitafanya hivyo.
“Lakini ukileta elimu ya bure nitakuunga mkono,” alisema Bw Owino.
Bw Owino alisema mfumo wa ufadhili wa masomo katika vyuo vikuu una ubaguzi akimsihi kuirekebisha ili kuwe na usawa.
Mbunge huyo alisema Rais hangelipiga hatua kubwa kimaisha ingalikuwa hakupelekwa shule huku akimsihi kusikia vilio vya Wakenya.
“Ulikutana na marehemu Rais Daniel Moi ulipokuwa chuo kikuu sababu ya elimu. Sasa umeleta mfumo mpya wa kufadhili elimu ya vyuo vikuu ambao una changamoto tele, unatekeleza mfumo wa CBC ambayo ina changamoto tele, hakuna maabara na kuna uhaba wa walimu,” akaongeza.
Kwenye kampeni za uchaguzi mkuu wa 2022, Rais aliapa kwamba ataondoa mfumo huo na kupiga msasa mfumo wa 8-4-4 lakini alipoingia mamlakani aliunda jopokazi la elimu ambalo lilichukua maoni kwa Wakenya.
Zaidi ya asilimia 90 ya Wakenya walikumbatia mfumo wa CBC.
“Ukifanya elimu iwe ya bure kuanzia shule za msingi hadi vyuo vikuu nitakuunga mkono,” akasisitiza.
Bw Owino alijinaki kuwa mwenyewe amewekeza kwenye sekta ya elimu kwa kujenga shule, kutoa basari kwa wanafunzi ili Wakenya wapate elimu bora.
Alisema wazazi wanapitia changamoto kulipa karo ya shule kwa watoto wao wanaosoma shule kutwa