Habari

Baraza la kijeshi Sudan latia saini makubaliano na makundi ya upinzani

July 17th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MASHIRIKA

KHARTOUM, SUDAN

BARAZA la Kijeshi linalotawala nchini Sudan kabla ya kukabidhi madaraka kwa utawala wa kiraia (TMC) na makundi ya upinzani wametia saini makubaliano ya ugavi wa mamlaka, mpatanishi wa Umoja wa Afrika (AU) amesema.

TMC na vuguvugu kubwa la upinzani Forces for Freedom and Change (FFC) wamekubaliana wawe wakipishana katika uongozi wa baraza linalojisimamia na kuongoza nchi hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu, amesema msuluhishi wa migogoro wa AU, Mohamed Hassan Ould Labat ambaye alihutubia wanahabari katika Corinthia Hotel jijini Khartoum ambako mgogoro huo umekuwa ukisuluhishwa.

Hatua hii inajiri siku kadhaa baada ya TMC na FFC kusema pande hizo zilikuwa zimefikia makubaliano kuhusu mpango wa kuelekea kuandaliwa uchaguzi nchini humo, ugavi wa mamlaka na uchunguzi wa machafuko ya hivi karibuni yaliyowalenga waandamanaji nchini na kusababisha vifo vya makumi ya watu.

Naibu mkuu wa baraza linalotawala, Mohamed Hamdan Dagalo na kiongozi wa muungano wa FFC, Ahmad al-Rabiah walitia saini makubaliano hayo mapema Julai 17, 2019, katika jiji hilo kuu.

Sasa makubaliano hayo yanatoa fursa kwa utawala wa kiraia ambao waandamanaji walitaka yakuwepo tangu kung’olewa kwa Rais Omar al-Bashir mnamo Aprili 2019.