BBI si njia ya Canaan – Wataalam
Na BENSON MATHEKA
AHADI za Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga kuwa mchakato wa kubadilisha katiba kupitia BBI unalenga kuimarisha maisha ya Wakenya ni hekaya tupu, ikizingatiwa kuwa watabebeshwa mzigo wa kuendesha serikali itakayobuniwa baada ya kura ya maamuzi.
Viongozi hao wamekuwa wakiambia Wakenya kwamba lengo lao la kuasisi mchakato huo ni kufanya Kenya kuwa Canaan, nchi yenye maendeleo na usawa waliokusudia waanzilishi wa taifa hili.
“Ninaona tukikaribia Canaan, kama Musa aliyeketi Mlima Nebali na kuona siku za usoni za wana wa Israeli walipokuwa karibu kuvuka hadi nchi ya ahadi; mimi pia nimeona siku zetu za usoni,” Rais Kenyatta alisema alipohutubia bunge.
Alisema anaona Kenya ambayo raia wake hawatasumbuliwa na umasikini kwa sababu ya utawala mbaya na ambayo rasilmali zitagawika kwa usawa ili nchi yote ipate ustawi.
Bw Odinga ambaye amekuwa akiahidi wafuasi wake kwamba atawaongoza hadi Canaan, pia alirejelea kauli hiyo wakati wa uzinduzi wa ukusanyaji saini za kuunga kura ya maamuzi mnamo Jumatano.
“Kuna nchi tunayoona. Tumetembea katika jangwa kwa muda mrefu. Tumetembea katika jangwa la njaa na kutengwa. Tunaweza kuona nchi ya ahadi mbele yetu,” Bw Odinga alisema.
Hata hivyo, mapendekezo ya ripoti hiyo ambayo yanaelekea kushirikishwa katika kura ya maamuzi yanaonyesha kuwa maisha ya mwananchi wa kawaida yatakuwa magumu baada ya uchaguzi mkuu ujao.
Mswada huo unapendekeza mageuzi muhimu yatekelezwe kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022. Ingawa Uhuru na Odinga wameahidi kwamba BBI ina mazuri, wadadisi wanasema Wakenya hawafai kutarajia Canaan baada ya kupitisha mswada wa BBI kwenye refarenda.
“Kuna mamba wengi katika BBI, haitavukisha Wakenya hadi Canaan bali wataendelea kubeba mzigo mzito wa kuendesha serikali itakayokuwa na nyadhifa nyingi kuliko ilivyo kwa sasa,” asema Lucia Ayiela wa vuguvugu la Kongamano la Mageuzi.
BBI inapendekeza nyadhifa tatu kuu zaidi za Waziri Mkuu na manaibu wawili. Imerejesha rasmi wadhifa wa mawaziri wasaidizi ambao watakuwa wabunge. Kwa sasa, katiba haitambui wadhifa huo ingawa Rais Kenyatta alitumia mamlaka yake kuwateua washirika wake wa kisiasa kusaidia mawaziri.
Gharama ya kuendesha serikali na lawama kuhusu mfumo wa ugavi wa rasilmali zimetambuliwa miongoni mwa masuala yatakayofanya ahadi za vinara wa BBI ya usawa na ustawi wa taifa kutotimia.
Katika mpangilio wa uongozi kwenye katiba ya 2010, serikali huwa inalalamika kuwa inatumia asilimia kubwa ya mapato yake kulipa mishahara, na wadadisi wanakadiria kuwa gharama hiyo itaongezeka maradufu mswada wa BBI ukipitishwa kwenye kura ya maamuzi.
Mswada huo unapendekeza viti vipya 70 vya ubunge ambavyo vikibuniwa vitaongeza gharama kwa mwananchi wa kawaida.
Kwa sasa kuna maeneobunge 290 na BBI ikipita Wakenya watalazimika kulipa wabunge 360 na maseneta 94. Kila kaunti itakuwa na maseneta wawili, mwanamume na mwanamke.
Kwa nchi ambayo inaendelea kulipa mlima wa madeni ya kigeni ya takriban Sh6.4 trilioni, maisha yatakuwa magumu nyadhifa hizi zitakapobuniwa Wakenya wakikubali BBI.
BBI inapendekeza serikali za kaunti zitengewe asilimia 35 ya mapato ya serikali ilhali inashindwa kutoa mgao wa sasa wa asilimia 15 kwa wakati.
“Ikiwa kaunti zimefilisika kwa kuwa serikali inashindwa kutoa asilimia 15 pekee ya pesa zinazotengewa, itakuwaje kwa asilimia 35? Hawa wabunge wanaoongezwa, manaibu waziri mkuu, na manaibu mawaziri watasaidia vipi kukomesha mizozo ya uchaguzi ambayo ndiyo chanzo cha fujo baada ya uchaguzi,” asema Mwanaharakati Ndungu Wainaina. Anasema kwamba kinyume na ahadi za vinara wa BBI, hali ya baadaye ya Wakenya itakuwa mbaya zaidi iwapo BBI itapitishwa.
“Wakenya, simameni mlinde nchi yenu, msinyamaze, simameni. Uchumi umedorora, hali ya afya ni duni, biashara zimeporomoka na ugatuzi umelemazwa kwa kunyimwa pesa,” alisema.
Pendekezo lingine ambalo litakuwa pigo kwa Wakenya wa kawaida na ambalo viongozi hao wamepigia debe ni kubuniwa kwa wadhifa wa kamishna wa kupiga darubini atakayeteuliwa na rais.
Kulingana na wadadisi, hatua hii itapokonya mahakama uhuru wake na iweze kutumiwa na viongozi kuidhinisha sera zake hata kama ni za kukandamiza raia.
Jana, Jaji Mkuu David Maraga aliwahimiza Wakenya kukataa pendekezo lolote linalonuiwa kupokonya mahakama uhuru wake.