BBI: Jinsi mambo yalivyokuwa Kitui
Na BONIFACE MWANIKI
MKUTANO wa uhamasisho wa mchakato wa maridhiano (BBI) uliofanyika Jumamosi katika Kaunti ya Kitui umehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo kiongozi wa ODM Raila Odinga ambaye amefika uwanjani akiwa kwa gari moja na Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Magavana.
Gavana wa Kaunti ya Makueni Prof Kivutha Kibwana amesoma mapendekezo ya eneo la Ukambani ambapo miongoni mwa mapendekezo yanahusu mji wa Konza, ustawishaji viwanda na uteuzi wa mawaziri katika ngazi za serikali ya kitaifa na zile za kaunti.
“Tunataka mji wa Konza ujengwe jinsi ulivyoratibiwa, viwanda vistawishwe katika eneo hili na mawaziri wawe wakiteuliwa baadhi kutoka nje ya waliopigiwa kura, lakini baadhi pia wawe ni kutoka kwa wale waliopigiwa kura na iwe hivi katika ngazi za serikali za kaunti na ya kitaifa,” amesoma Kibwana.
Kibwana pia amesoma mapendekezo ya eneo akisema ipo haja kustawisha sekta ya uzalishaji kawi; hasa kutoka kwa jua.
“Tungependa nafasi kuu za uongozi nchini ziongezwe ili kuwe na Waziri Mkuu mwenye mamlaka na fedha zaidi ziweze kutengewa ugatuzi,” ikasema sehemu moja ya mapendekezo yaliyotolewa na viongozi wa eneo la Ukambani.
Viongozi wengi waliozungumza wamewataka wakazi kuunga mkono juhudi za Rais Uhuru Kenyatta na Raila za kuwaleta Wakenya pamoja.
Hafla hii pia imewaleta pamoja wambunge zaidi ya 15 kutoka eneo la Ukambani na magavana, maseneta na viongozi wengine kutoka maeneo tofauti nchini.
Raila amesema kuwa viongozi wanaounga mkono mchakato wa BBI wataendelea kuzuru maeneo zaidi hapa nchini ikiwemo maeneo ya Meru, Narok, Nakuru na Nairobi ili kuhakikisha kuwa mabadiliko yatakayoboresha taifa la Kenya yanapatikana na yanaafikiwa.
“Tutaendelea kupeleka mchakato wa BBI katika maeneo tofauti nchini, ikiwemo; kaunti za Meru, Narok, Garissa, na Nakuru ili kuhakikisha kuwa Wakenya wote wanahusishwa kwenye suala hili,” amesema Raila.
Amesema madhumuni ya mchakato wa BBI ni kuleta mabadiliko nchini; ikiwemo kutengeza nafasi zaidi za kazi kwa vijana, kuleta uwiano nchini na kuzuia umwagikaji wa damu kila baada ya uchanguzi.
“Nia iliyotuleta pamoja mimi na Rais Uhuru Kenyatta ilikuwa ni kuwaleta Wakenya wote pamoja na kuhakikisha kuwa hakuna umwagikaji zaidi wa damu kila baada ya uchanguzi nchini,” ameongeza kiongozi huyu wa upinzani.
Amewaonya viongozi wote ambao hawaungi mkono juhudi za BBI, akisema kuwa hawatoweza kuzuia swala muhimu kama hili.
“Hakuna yeyote atakayefanikiwa kuzuia mchakato wa BBI. Wanaotafuta njia za kupinga suala muhimu kama hili ningependa kuwaaambia ole wao!” amesema.
Naye Kalonzo amesisitiza maoni yake ya kutaka magavana wakubaliwe kuomba kiti cha ugavana mara nyingi iwezekanavyo bila kuweka hatamu maalum ya uongozi.
“Najua wengi hawakuelewa pendekezo langu; nilililosema lilikuwa tu magavana nchini wanafaa kupewa nafasi zaidi za kuomba kiti hicho na iwapo wakazi wa maeneo ya wanakotoka hawatakuwa wameridhishwa na utawala wao, hawatokuwa na budi kuwabandua uongozini,” ameeleza Bw Musyoka.
Aidha, kiongozi huyo wa Chama cha Wiper amewataka viongozi nchini kutumia BBI kuwaunganisha Wakenya pamoja, na wala si kutafuta mgawanyiko.
“Ningewasihi viongozi wote nchini kutumia fursa hii kuwaleta Wakenya pamoja na kwamba asitokee yeyote akaja akazua uhasama miongoni mwao,” amesisitiza Musyoka.
Musyoka amewashukuru viongozi wote wa ukambani kwa kuungana pamoja ili kufanikisha mkutano wa BBI mjini Kitui na kuwataka waungane hivyo tena kwa mkutano mwingine unaonuiwa kuandaliwa katika eneo la Wote katika Kaunti ya Makueni.
Kwenye mapendekezo ya viongozi wanawake nchini yaliyosomwa na Spika wa Kaunti ya Nairobi Bi Beatrice Elachi, wanawake nchini wametaka kutekelezwa kwa kipengele cha kuhakika 2/3 ya kila jinsia katika kila sekta ya umma almaarufu (Two thirds gender rule).
“Tungapenda swala la usawa wa kijinsia liangaziwe vizuri kwenye BBI ili kipengele cha katiba cha thuluthi mbili kitekelezwe ipasavyo,” amesoma Bi Elachi.
Viongozi hawa pia walisema kuwa wanaunga mkono ugatuzi na wakapendekeza kuongezwa mgao wa fedha unaopatika magatuzi kutoka asilimia 15 sasa, hadi asilimia 45 ili kuhakikisha kutekelezwa kwa miradi zaidi ya maendeleo nchini.
Mapendekezo ya viongozi hawa yalikabidhiwa kinara wa Upinzani Bwana Raila Odinga ili kuongezewa kwenye ripoti ya BBI.
Gavana mwenyeji, Ngilu kwa upande wake amependekeza nafasi za viongozi wanawake kuongezwa nchini, akisema kuwa wakazi wa Kitui wanaunga mkono mchakato wa BBI mia kwa mia.
“Ningependa kukukuhakikishia kuwa wakaazi wa eneo nzima la Ukambani wako nyuma ya BBI na kuwa tunaunga mkono juhudi za kuwaleta wakenya pamoja,” alisema Bi Ngilu.
Mapema wasafiri katika matatu yenye uwezo wa kubeba abiria 45 iliyosombwa na maji ya Mto Waani uliovunja kingo zake katika barabara ya Itangini-Tawa wamepata usafiri mbadala hadi Kaunti ya Kitui kuhudhuria mkutano huo (BBI).
Abiria hao walikuwa wanatoka katika Kaunti ya Makueni.
Kulikuwa na kizaazaa Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria alipofurushwa kutoka kwa mkutano wa uhamasisho wa BBI katika Kaunti ya Kitui.
Gavana mwenyeji Charity Ngilu alisikika akisema hataruhusu “viongozi wa matusi.”
Hata hivyo Kuria aliruhusiwa kurudi uwanjani na utulivu kurejea baada ya makamu wa Rais wa zamani Kalonzo Musyoka na Raila kuingilia kati.
Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen ambaye ni Mwandani wa Naibu Rais William Ruto pia amehudhuria mkutano huo.