Habari

BBI yatawala Jamhuri

December 13th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CECIL ODONGO

RAIS Uhuru Kenyatta jana alitumia maadhimisho ya sherehe za Sikukuu ya Jamhuri kupigia upatu ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) akisema mabadiliko ya katiba yatakayofanyika yanalenga kuweka taifa kwenye mkondo salama kisiasa na kiuchumi.

Ripoti hiyo ni matokeo ya muafaka wa kisiasa kati ya Rais Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga mnamo Machi 9, 2018 na imezua mdahalo mkubwa nchini kati ya mirengo mbalimbali ya kisiasa.

Kiongozi wa nchi na Bw Odinga nao wamekuwa wakivumisha ripoti hiyo wakisema kuwa ni kamilifu na muhimu zaidi kwa kuwa inashughulikia masuala muhimu ambayo yanalenga umoja wa nchi. Wawili hao wamewataka Wakenya wapitishe BBI jinsi ilivyoandikwa na wanakamati bila kufanyiwa mabadiliko ya ziada.

Kwa upande mwingine, Naibu Rais, Dkt William Ruto naye amekuwa akisisitiza kuwa BBI inafaa kuyajumuisha maoni ya wote ili patakapoandaliwa kura ya maamuzi, taifa lisigawanyike katika mirengo ya ‘La’ na ‘Ndiyo’.

Tayari saini za kuunga BBI zimekabidhiwa Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ili zikaguliwe kabla ya kuandaliwa kwa kura ya maamuzi.

Rais aliyeongoza sherehe hizo katika uwanja wa kitaifa wa Nyayo, alisisitiza kuwa BBI ndiyo suluhu, si tu kwa migogoro ya kisiasa ambayo imekuwa ikitokea nchini kila mwaka wa uchaguzi, bali pia inajumuisha masuala ambayo yamelalamikiwa kwa miaka mingi.

“BBI inapendekeza marekebisho ya katiba ambayo yatahakikisha kuwa taifa letu linapiga hatua katika nyanja mbalimbali. Ripoti hiyo inalenga kuhakikisha kuwa tunamaliza safari tuliyoianza baada ya kurasimisha katiba mpya,” akasema Rais Kenyatta.

Rais aliwakumbusha Wakenya kuwa aliyekuwa Katibu wa Umoja wa Mataifa, marehemu Koffi Annan mnamo 2008 aliwarai viongozi wabadilishe katiba ambayo inagatua mamlaka ili wanaopoteza uchaguzi hawaachwi nje ya uongozi.

Ripoti ya BBI inapendekeza kubuniwa kwa nafas ya waziri mkuu, manaibu wake wawili na afisi ya kiongozi wa upinzani ambayo itafadhiliwa na serikali iliyoko mamlakani.

“Kuongezwa kwa nafasi za uongozi kupitia kubuniwa kwa afisi ya Waziri Mkuu na manaibu wake wawili ni suala lililopitishwa wakati wa vikao vya upatanishi baada ya uchaguzi tata wa 2007. Iwapo matokeo yake yalifanya kazi na amani ikadumu kwa nini tusifanye hivyo kwa sasa?” akauliza Rais.

“Kama kiongozi wa upinzani anajivunia ufuasi mkubwa na mshindi wa uchaguzi pia ana umaarufu, basi njia pekee ya kuleta umoja ni kufadhili afisi ya kinara wa upinzani na baraza lake la mawaziri,” akaongeza Rais.

Vilevile alisifia BBI akisema itahakikisha mgogoro kuhusu usawa wa kijinsia ambao umekwepo kwa muda mrefu unasuluhishwa wanawake 47 wakichaguliwa kwenye Bunge la Seneti.

Rais alisisitiza kuwa maoni ya wanawake yatasikizwa kuhusu masuala mbalimbali kupitia bunge la seneti kinyume na sasa ambapo wanashikilia nafasi chache mno.

Pia alisifu BBI kwa kuongeza mgao kwa serikali za kaunti kwa asilimia 35 na kutenga hazina ya maendeleo ya wadi.

Kinyume na sherehe zilizopita za kitaifa ambapo Naibu Rais alimwalika Bw Odinga kuhutubu kisha kumkaribisha Rais, jana hilo halikufanyika, Dkt Ruto alimwalika Rais Kenyatta moja kwa moja.

Rais Kenyatta pia alitetea kubuniwa kwa afisi inayotetea maslahi ya umma (Ombudsman) kuhakikisha kuwa idara ya mahakama inawatendea raia haki.

Mnamo Ijumaa Jaji Mkuu anayeondoka, Bw David Maraga alisema wanaohudumu katika afisi hiyo wanafaa kuteuliwa na Tume ya Huduma ya Mahakama (JSC) wala si afisi ya Rais jinsi ilivyopendekezwa katika ripoti ya BBI.

Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ya kitaifa ni makamau wa rais wa zamani Kalonzo Musyoka ambaye ni kiongozi wa chama cha Wiper, mwenzake aliyehudumu katika wadhifa huo, Bw Musalia Mudavadi (ANC) na Moses Wetang’ula (Ford Kenya).