Biashara ya mitihani bandia yazidi kuwaumiza wazazi
WAZAZI wanaendelea kutumia maelfu ya pesa kununua karatasi za mazoezi na mitihani ya kutabiri maswali yanayoweza kutokea katika mitihani ya kitaifa, hali inayoongeza mzigo kwa familia zinazokabiliwa na gharama kubwa ya maisha.
Biashara hiyo inahusisha karatasi za kutabiri maswali, mitihani ya majaribio, majibu na vikundi vya WhatsApp vinavyotoza ada kwa wanafunzi wanaotaka kujiandaa kwa mitihani.
Uchunguzi umebaini kuwa baadhi ya wauzaji huchapisha karatasi wakidai zimetoka shule maarufu kama Alliance High School, Maranda High School na The Kenya High School, wakitumia sifa za shule hizo kuwashawishi wazazi kuzinunua.
Hata hivyo, si rahisi kuthibitisha uhalisi wa karatasi hizo, huku baadhi ya mazoezi yakiwa hayajaidhinishwa na Taasisi ya Ukuzaji Mitaala nchini (KICD).
Zaidi ya wanafunzi 3.6 milioni wanatarajiwa kufanya tathmini na mitihani ya kitaifa mwaka huu. Kati yao, 1,380,463 watafanya tathmini ya shule za msingi (KPSEA), 1,206,028 tathmini ya Sekondari Msingi (KJSEA), huku 1,048,355 wakifanya mtihani wa KCSE.
Wauzaji hutangaza karatasi za mazoezi kwa bei ya kuanzia Sh100 hadi maelfu ya shilingi, kutegemea muda wa usajili na aina ya nyenzo zinazotolewa.
Baadhi ya majukwaa ya mtandaoni hutoza Sh290 kwa saa 24 za matumizi, Sh590 kwa mwezi, Sh940 kwa miezi sita na Sh1,480 kwa mwaka.
Mzazi mmoja ambaye mtoto wake anafanya KCSE alisema gharama inaongezeka kila anaponunua kifurushi kipya cha karatasi hizo.
“Kila unapofikiria kuwa umemaliza kulipia mahitaji yote, kifurushi kingine cha mazoezi kinatokea. Unaambiwa hiki kina maswali bora zaidi au wanafunzi wengine wanakitumia. Unaogopa kumnyima mtoto wako kitu kinachoweza kumsaidia,” alisema.
Mzazi mwingine alisema tayari alikuwa amenunua vitabu na mitihani ya zamani, lakini mtoto wake aliendelea kuomba karatasi zinazosambazwa katika vikundi vya WhatsApp.
Wadau wa elimu wanaonya kuwa baadhi ya wauzaji wanatumia hofu ya wazazi kwa kuahidi kutabiri maswali yatakayotokea katika mitihani halisi.
Mkuu wa Baraza la Mitihani nchini (KNEC), Dkt David Njengere, amewahi kuwaonya wazazi dhidi ya kununua karatasi hizo, akisema ni kupoteza muda na pesa.
Mwalimu mkuu mmoja alisema kununua vifurushi vingi hakumaanishi mwanafunzi atapata alama za juu.
“Mwanafunzi aliyejiandaa vizuri kwa kutumia mitihani ya zamani, vitabu na nyenzo zinazotolewa na walimu anaweza kufanya vizuri bila kununua karatasi nyingi zizothibitishwa,” alisema.
Alionya kuwa biashara hiyo inawafanya wanafunzi kuamini kuwa hawawezi kufaulu bila kununua karatasi fulani, jambo linaloongeza wasiwasi kwa watoto ambao wazazi wao hawana uwezo wa kuzilipia.
Wakati huo huo, Waziri wa Elimu Julius Ogamba ameonya kuwa watahiniwa na maafisa watakaopatikana wakijihusisha na udanganyifu wa mitihani watachukuliwa hatua kali za kisheria.
KNEC pia imewaonya wazazi dhidi ya matapeli wanaodai kuwa na mitihani iliyovuja kabla ya kufanywa, ikisema wengi huuza karatasi bandia kwa familia zisizokuwa na habari.