Bila Raila wa kuning’inia, Orengo atachukua mwelekeo upi kisiasa?
WENGI sasa wanasubiri kufahamu mwelekeo wa kisiasa ambao Gavana wa Siaya James Orengo atachukua baada ya kuendelea kuasi msimamo wa ODM wa kushirikiana na Serikali Jumuishi.
Novemba 14, 2025, wakati wa maadhimisho ya miaka 20 ya ODM jijini Mombasa, Bw Orengo alichemsha kwa kudai kuwa Rais William Ruto ndiye anahitaji ODM kuliko jinsi ambavyo chama hicho kinamhitaji.
Bw Orengo yupo kwenye tapo la viongozi ambao wanapinga ODM kuendelea kushirikiana na Rais Ruto.
“Tunahitaji serikali ambayo inawajibika na tunavyozungumza sasa, sina hofu kusema kuwa Ruto anahitaji ODM na si ODM ndiyo inahitaji Ruto. Sijui mnanisikia. Kuna watu hapa wanajifanya kana kwamba ni ODM ndiyo inahitaji Ruto,” akasema Bw Orengo.
“Mniambie 2027 mkimpa Ruto urais, ODM inabakia wapi? Huwezi kuzunguka kote nchini na kuwaambia wananchi kuwa utakuwa serikali au sehemu ya serikali. Chama imara lazima kifahamu kile ambacho kinataka,” akaongeza.
Gavana huyo alisema kuwa mwenyewe yupo tayari kurejea barabarani kushiriki maandamano iwapo utawala wa sasa utaendelea kuwanyanyasa raia.
Licha ya kuonyesha ukakamavu Mombasa na kuwateka hadhira kwa kushambulia Rais Ruto, masuali yameibuka mwelekeo wa kisiasa ambao Bw Orengo sasa atachukua hasa baada ya mauti ya Kinara wa ODM Raila Odinga.
Wakati wa uhai wa Raila, Bw Orengo pia alikuwa vuguvugu kuhusu Serikali Jumuishi lakini akanyoosha moyo baada ya kukosolewa na viongozi wengi wa sasa akiwemo Kinara wa sasa wa ODM Dkt Oburu Oginga.
Tamko la kurejea maandamano alilolotoa Bw Orengo halikupokelewa na viongozi wanaoegemea mrengo wa serikali kutoka Nyanza pamoja na viongozi wa kidini ambao walisema eneo hilo limepitia madhila katika maandamano ya hapo awali.
“Viongozi wanastahili kukoma kuwachochea raia kurudi maandamano kwa sababu Raila alituacha serikalini hadi 2027. Kwa sasa tunastahili kumakinikia miradi ambayo ilianzishwa na utawala huu hadi ukamilishwe badala ya kuingiza siasa,” akasema Askofu Washington Ogonyo Ngede wa Kanisa la Power of Jesus akiongea na idhaa ya Nam Lolwe Jumamosi iliyopita.
Dkt Oginga mwenyewe aliashiria kuwa Nyanza haiko tayari kurejea kwenye maandamano alipokuwa mwenyeji wa Rais Ruto kwenye dhifa ya kuenzi ODM.
Japo Bw Orengo ni mkakamavu mbele ya umma, nyumbani huenda akakabiliwa na kibarua cha kutetea kiti chake hasa iwapo Serikali Jumuishi itaendelea kushabikiwa na wakati huu ambapo Raila.
Marehemu Raila amekuwa akimbeba Bw Orengo mgongoni kisiasa tangu 2007 alipomwondoa kwenye baridi na akafanikisha ushindi wake kama mbunge wa Ugenya licha ya upinzani kali kutoka kwa Steve Mwanga.
Gavana huyo alishinda chaguzi za 2007, 2013, 2017 na 2022 kutokana nguvu za Raila na ODM. Mnamo 2022, Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi alishawishiwa kutupa azma yake ya ugavana na kurejelea kiti chake cha ubunge ili kumpisha Bw Orengo awanie ugavana.
Pia matokeo mbalimbali ya kampuni za utafiti yamekuwa yakionyesha kuwa gavana huyo ana utendakazi usioridhisha, hii ikifanya kazi kuwa ngumu zaidi kwake 2027.
Aidha kiny’ang’anyiro cha ugavana Siaya kimeanza kupamba moto huku Mbunge wa Ugenya David Ochieng’, Mbunge wa zamani wa Rarieda Nicholas Gumbo wakitarajiwa kukabiliana na Bw Orengo.
Minong’ono pia inaashiria kuwa Bw Wandayi pia huenda akawania kiti hicho.
Wakati Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka alipotembelea Opoda, Bw Orengo alimsifu kwa kusimama na Raila kwenye chaguzi tatu zilizopita, kauli ambayo ilifasiriwa kuwa huenda anachangamkia mrengo wa upinzani.
“Wale wote ambao walikuwa wakining’inia Raila hawatapata viti vyao kirahisi akiwemo Oburu. Kwa hivyo, ni mapema sana kusema kuwa Orengo atashinda au kushindwa, shida pekee ni kwamba amekuwa na utendakazi duni. Hata hivyo, hii haishangazi kwa sababu yeye ni mwanaharakati badala ya mchapa kazi,” akasema Bw Andati.