Habari

Bima ya bodaboda kuwakinga abiria itaumiza wahudumu – wabunge

June 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wamepinga pendekezo la serikali kwamba waendeshaji pikipiki za uchukuzi – bodaboda – watahitaji kuchukua bima ya kuwakinga abiria wao dhidi ya madhara kama vile ajali za kila mara.

Walisema hatua hiyo itaua sekta hiyo ambayo imekuwa tegemeo kuu kwa Wakenya wasio na ajira zinginezo za kuwafaa, hususan, vijana.

Kulingana na viongozi hao, wazo hilo lililotangazwa na Waziri wa Fedha Henry Rotich alipowasilisha taarifa ya bajeti bungeni Alhamisi, huenda likachangia kuzorota kwa usalama nchini.

Hii ni kwa sababu wale ambao watalazimika kuacha biashara ya bodaboda kwa kushindwa kugharimia bima hiyo huenda wakaamua kujiingiza kwenye uhalifu “kujitafutia riziki.”

“Tunapaswa kuangalia upya suala hili. Kutaka waendeshaji bodaboda kulipa ada zaidi za bima kuwakimu wateja wao ni kuwaumiza zaidi vijana hawa. Wakishindwa kugharimia bima hii bila shaka wataacha biashara hiyo na baadhi kugeukia uhalifu kama njia mbadala ya kujichumia pato,” akasema Mbunge wa Kiminini Chris Wamalwa Alhamisi jioni baada ya kusomwa kwa taarifa ya bajeti.

‘Mambo yawe kama zamani’

Naye Mbunge wa Kieni Kanini Kega alimtaka Waziri Rotich kufutilia mbali hitaji hilo la bima na kuwaruhusu wanabodaboda kuendesha biashara yao kama zamani.

“Hawa ni watu ambao huingiza kati ya Sh300 na Sh800 kwa siku. Sasa watapata wapi pesa za kulipia abiria wao bima. Hii ni njia ya kuuwa sekta hii ambayo imekuwa ikitoa ajira kwa vijana wetu ambao hawana ajira licha baadhi ya kusoma hadi viwango vya vyuo vikuu,” akasema Mbunge huyo ambaye ni mwenyekiti wa Kamati kuhusu Biashara na Ustawi wa Viwanda.

Wengine waliopinga pendekezo hilo la Bw Rotich ni George Aladwa (Makadara), Hillary Kosgei (Kipkelion Magharibi), Simba Arati (Dagoreti Kaskazini) na Elisha Odhiambo (Gem).

Hata hivyo, akitetea pendekezo hilo, Bw Rotich alisema bima hiyo itasaidia kugharamia watibabu ya wananchi wengi ambao wamekuwa wakijeruhiwa katika ajali zinazohusisha bodaboda hizi kila mara.

“Kuna haja ya kulinda abiria wa bodaboda dhidi ya ajali ambazo zimekuwa zikishuhudiwa katika sekta hii kila mara. Ili kufanikisha hilo, wahudumu hao sasa watahitaji kulipia abiria wao bima,” akasema Rotich.

Bw Rotich alieleza kuwa ingawa sekta hiyo imeajiri vijana wengi kwa sababu hutumiwa na watu wengi, pikipiki hizo husababisha ajali nyingi ambazo zimeacha watu wengi na majeraha ya kudumu na hata ulemavu.