Bloga mashakani kwa kumtukana Kidero ‘matusi meusi’
MWANABLOGA aliyeshtakiwa Jumatatu kwa kumtukana aliyekuwa Gavana wa Nairobi Dkt Evans Kidero alishtuka pale hakimu alipomweleza anakodolewa macho na kifungo cha miaka 20 gerezani akipatikana na hatia.
Bonface Omondi Nyangla aliduwaa zaidi kuelezwa na hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Dolphina Alego kwamba matusi aliyopeperusha katika mtandao wa Facebook yataacha pengo ya Sh10 milioni katika akaunti yake kwa vile sheria inaamuru watukanaji katika mitandao watozwe faini hiyo ama pia waadhibiwe kifungo cha jela na wakati huo huo kulipa faini.
Nyangla, alishtuka alipofahamishwa hayo na hakimu Alego, kwamba “adhabu ya makosa uliyofanya ya kumtusi na kumdhalilisha na kumshushia hadhi Dkt Kidero ni kifungo cha miaka 20 gerezani ama atozwe faini ya Sh10 milioni ama vyote viwili.”
Nyangla alishtakiwa kuchapisha katika mtandao wa Facebook matusi ambayo hatuwezi kuchapisha katika Taifa Leo kwa sababu ya kutunza hadhi na heshima ya wasomaji na mlalamishi.
Nyangla alishtakiwa kupeperusha matusi hayo ya kumshushia heshima Dkt Kidero katika mtandao wake Aprili 20, 2025.
“Kabla sijaamua kiwango cha dhamana nitakayokuachilia nayo, nataka kukueleza kwamba adhabu ya makosa uliyofanya ni kifungo cha miaka 20 gerezani ama faini ya Sh10 milioni. Pia mahakama inaweza kuamua kukuadhibu kifungo na faini,” Bi Alego alimweleza Nyangla.
Hakimu aliongeza kumweleza kwamba dhamana anayoweza kupewa ya kiwango cha chini kabisa ni Sh1 milioni.
Akimlilia hakimu, Nyangla mwenye umri wa miaka 40 na mfanyakazi wa Kenya National Trading Corporation (KNTC), alifungua roho na kusema “niko na watoto wanaorudi shule Aprili 29, 2025 na tangu nikamatwe na kuzuiliwa kwa siku tano hakuna mipango yoyote nimefanya ya kuwarudisha shuleni na vyuoni.”
Mshtakiwa alimsihi hakimu amwonee huruma kwa sababu ya watoto.
Alisema alikamatwa wakati familia yake imeenda nyumbani kwa sherehe za Pasaka na hawajui aliko kwa vile maafisa wa polisi wa uchunguzi wa jinai (DCI) walimnyang’anya simu na kumzuilia katika kituo cha polisi cha Kamkunji.
Bi Alego alimwachilia Nyangla kwa dhamana ya Sh1 milioni na mdhamini mmoja wa kiasi sawa na hicho.
Pia alipewa dhamana ya Sh400,000 pesa tasilimu.
Mbali na masharti hayo, hakimu aliamuru idara ya urekebishaji tabia imhoji mshtakiwa na kuwasilisha ripoti yake Mei 6, 2025 ndipo atathmini ikiwa atampunguzia dhamana au la.
Mshtakiwa aliyekuwa mpigia debe Dkt Kidero wakati wa kampeini za uchaguzi mkuu uliopita alirudishwa rumande kwa vile hakuweza kulipa dhamana hiyo mara moja.