Habari

Bodi ya maziwa yatangaza kusitisha 'sheria dhalilishi'

March 26th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Wafugaji: Sheria za kudhibiti maziwa zitatukandamiza

Sheria za kudhibiti uuzaji wa maziwa nchini zinaendelea kuzua hisia tofauti miongoni mwa wafugaji wa ng’ombe wa maziwa.

Ingawa bodi ya maziwa nchini, KDB, Jumatatu ilitangaza kusimamishwa kwa muda utekelezwaji wake, sheria hizo zinapendekeza maziwa kupata hifadhi maalum hasa kupitia waliodhinishwa na bodi hiyo kabla ya kuuzwa. Hii ina maana kuwa maziwa yanayopaswa kuuzwa ni yaliyosindikwa.

Kwa mujibu wa sheria hizo, mfugaji anaonywa kutouzia mteja; jirani au wachuuzi, maziwa moja kwa moja. Walioidhinishwa na KDB ndio anapaswa kuwauzia.

Ng’ombe wa kuzalisha maziwa wakikamwa kupitia mitambo ya kisasa. Picha/ Sammy Waweru

Mwae Malibet, mfugaji eneo la Gachie, Kiambu analalamikia sheria hizi akihoji zimelenga kumkandamiza mkulima, hasa yule ndogo. Ikizingatiwa kwamba wengi nchini wanategemea biashara ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, mfugaji huyu anashangaa watakapoenda walioajiriwa kupitia sekta hii.

“Zikitekelezwa zilivyo, wengi wetu tutapoteza ajira. Tunategemea mapato ya uuzaji wa maziwa kutoka kwa ng’ombe mmoja, wawili au watatu,” anateta Bw Malibet.

Kulingana na Bw Stephen Mathenge, mfugaji Kirinyaga, pendekezo la hifadhi maalum ni gharama kwa mkulima kwa sababu atalazimika kuwa na mashine, zinazomhitaji kuwa na leseni.

“Tunapoyakama, huyauza moja kwa moja yakiwa salama. Mkondo wa sheria hizo utafungia wengi nje, kilele chake kikiwa kuacha ufugaji,” Mathenge akaambia Taifa Leo Digitali wakati wa mahojiano.

Viwanda vya kununua maziwa na kusindika, vinaruhusiwa kuyaagiza kutoka nje ya nchi endapo vitahisi kuna upungufu wa bidhaa hii. Kemikali hutumika kusindika bidhaa za kula au kunywa, na ni wazi itakuwa changamoto kwa watoto wadogo kuyanywa. “Ingekuwa busara ikiwa serikali itatathmini sheria hizo kwa kina, kwa minajili pia ya watoto ambao hawajafikia umri wa kula na hutegemea maziwa ya mama na ng’ombe pekee,” anashauri Purity Gathogo, mfugaji Nyeri.

Aidha, sheria hizo zinapendekeza wakiukaji kuadhibiwa faini ya Sh500,000 kila mmoja ama kuhudumu kifungu cha miaka miwili gerezani, au adhabu zote mbili.

Akitoa tangazo la kusitisha utekelezwaji wake kwa muda, meneja mkuu wa KDB Bi Margaret Kibogy, alisema bodi hiyo itashirikisha maoni ya wafugaji na wadau husika.

Baadhi ya wabunge wanaotoka maeneo ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa, wametishia kuurambisha sakafu mswada wa sheria hizo ukiwasilishwa bungeni ulivyo.