Boyd, Aroko wafanya ODM ijikune kichwa uchaguzi mdogo wa Kasipul
CHAMA cha ODM kinakabiliwa na mtihani mkubwa wa kumteua mwaniaji wa kiti cha ubunge Kasipul, Kaunti ya Homa Bay kwenye uchaguzi mdogo eneo hilo.
Kiti hicho kilisalia wazi baada ya kifo cha Charles Ongóndo Were jijini Nairobi mnamo Aprili 30.
Kuna ushindani mkali ambao umeibuka kati ya wawaniaji watatu ambao wanamezea mate kiti hicho.
Wao ni Boyd Were, mwanawe marehemu mbunge, mfanyabiashara mwenye mfuko mzito Philip Aroko na Robert Riaga ambaye anafahamika kama Money Bior kutokana na ukwasi wake.
Watatu hao wamekuwa wakiendeleza kampeni kali mashinani japo Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) bado haijatangaza siku ya kuandaliwa kwa uchaguzi huo mdogo.
Bw Riaga ametangaza kuwa atawania kama mgombeaji huru na amekuwa akitumia rangi ya samawati kama nembo yake.
Kati ya mbinu zake ni kushiriki miradi mbalimbali pamoja na kulipa bili ya hospitali na karo kwa wanafunzi kutoka familia ambazo hazijiwezi.
Bw Aroko na Bw Were wanawania tikiti ya ODM na inaonekana kuwa atakayeshinda mchujo wa chama hicho yupo pazuri kutwaa kiti cha ubunge ikizingatiwa ODM ni maarufu mno eneo hilo.
ODM imekuwa ikitumia mchujo au kutoa tikiti ya moja kwa moja kwa wawaniaji wake na inatazamiwa kuonwa itatumia mbinu gani Kasipul.
Tatizo ni kuwa utoaji wa tikiti ya moja kwa moja umewahi kuponza ODM baada ya baadhi ya wawaniaji kuamua kusimama kama wagombeaji huru.
Wakazi wengi sasa wanapendekeza ODM itumie uteuzi kwa njia ya wazi ili mwaniaji huru apeperushe bendera ya nchi.
“Chama kitapoteza umaarufu wake iwapo raia hawatapewa nafasi ya kumchagua mwaniaji ambaye wanampenda. Mchakato wa uteuzi ukiwa huru basi hatuna shida na mwaniaji wa ODM,” akasema mkazi wa Kasipul, Wycliffe Ochieng’
Mkazi mwengine alionya kuwa kutakuwa na taharuki ya kisiasa iwapo ODM itapendelea mwaniaji mmoja.
“Kuna madai kuwa chama tayari kina mwaniaji wake na hii inasababisha wafuasi wa wawaniaji wengine waingiwe na wasiwasi,” akasema mkazi huyo Leonard Oluoch.
Wachanganuzi wa kisiasa nao wanataka wakazi wawachague viongozi wachapa kazi badala ya uaminifu kwa chama.
Mchanganuzi wa masuala ya Michael Koja amesema anayestahili kuchaguliwa ni yule atakayeimarisha maisha ya wakazi wa Kasipul badala ya kumakinikia tu uaminifu kwa chama.
Bw Aroko amekuwa akisisitiza kuwa yeye ni mwanachama wa ODM na akakanusha madai yanayoenezwa na yanamhusisha na UDA.
“Sitatishwa kwa sababu nafanya kile naona ni kizuri,” akasema.
Alirejea kwenye eneobunge hilo wiki jana baada ya siku kadhaa kutokana na uchunguzi uliokuwa ukiendelea wa kumhusisha na mauaji ya marehemu Were.
“Mimi ni mweupe kama pamba na sote lazima tuungane kuhakikisha Kasipul inavutia wawekezaji na ina amani,” akasema Bw Aroko wakati wa kukaribishwa kwake nyumbani wiki jana.
“Wapigakura wa Kasipul lazima wapewe uhuru wa kumchagua mwakilishi wao bila kuingiliwa,” akasema.
Alizindua kampeni yake kwenye soko la Ombek kisha akaendeleza mikutano barabara ya Oyugis-Rodi Kopany kabla ya kuhitimisha kwa mkutano wa kisiasa nyumbani kwake Kamagak Mashariki.
Mfanyabiashara huyo alikuwa akilenga kupambana debeni na marehemu Were mnamo 2027.
Hata hivyo, sasa atapambana na Bw Boyd ambaye amekuwa akiungwa mkono na viongozi wakuu wa ODM akiwemo Mwenyekiti wa chama na Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga.