Breki nyingine: Jaji azima mswada wa CDF kupelekwa kwa Ruto
MAHAKAMA Kuu imezuia Bunge kuwasilisha Mswada wa Marekebisho ya Katiba ya Kenya wa mwaka 2025 kwa Rais William Ruto ili autie saini kuwa sheria.
Jaji wa Mahakama Kuu, Lawrence Mugambi, alitaja maslahi ya umma katika kusimamisha mchakato huo kwa sababu mara tu mswada huo, ambao bado unasubiri kupitishwa na Seneti utakapotiwa saini kuwa sheria, hautaweza kubatilishwa isipokuwa kwa marekebisho mengine ya katiba.
Mswada huo, ambao umefadhiliwa na Mbunge wa Rarieda Otiende Amollo na Mbunge wa Ainabkoi Samuel Chepkonga, unalenga kukita katika katiba hazina tatu muhimu: Hazina ya Maeneobunge ya Serikali Kuu (NG-CDF), Hazina ya Usimamizi ya Seneti (SOF), na Hazina ya Uwezeshaji wa Jinsia ya Serikali Kuu (NG-AAF).
“Kabla ya kusikizwa na kuamuliwa kwa kesi hii, amri ya muda inatolewa kuzuia kuwasilishwa kwa Mswada wa Marekebisho ya Katiba kwa Rais ili autie saini. Iwapo utasainiwa, hautaanza kutekelezwa hadi kesi isikizwe na kuamuliwa,” alisema jaji huyo.
Wabunge waliupitisha mswada huo kwa kauli moja uliposomwa mara ya pili kwa kura 304, na kwa kura 298 uliposomwa mara tatu.
Baada ya kupitishwa na Bunge la Kitaifa, mswada huo ulipelekwa Seneti kujadiliwa na kuidhinishwa.
Hata hivyo, mashirika kadhaa ya kutetea haki yalipinga mswada huo yakidai kuwa Bunge lilianzisha mchakato wa kurekebisha katiba bila kutunga sheria ya kura ya maamuzi itakayoongoza mchakato huo.
Walalamishi walisema kuwa mswada huo ni hadaa kwa sababu NG-CDF ilitangazwa kinyume cha kikatiba na Mahakama Kuu, Mahakama ya Rufaa na Mahakama ya Juu zaidi.
Mwaka jana, jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu lilitangaza kuwa Sheria ya NG-CDF si halali kikatiba kwa kuwa inakiuka dhana ya kutenganisha mamlaka.
Mahakama iliamua kuwa NG-CDF pamoja na miradi, mipango na shughuli zake zote zitasitishwa rasmi ifikapo saa sita usiku wa Juni 30, 2026.
Bunge na Mwanasheria Mkuu waliwasilisha pingamizi la awali wakisema kuwa walalamishi walipaswa kuwasilisha maoni yao kwa mabunge yote mawili kabla ya kufika mahakamani.
Mwanasheria Mkuu aliongeza kuwa mahakama haina mamlaka ya kuamua kesi hiyo kwa mujibu wa dhana ya kutanganisha mamlaka kati ya mihimili ya serikali.
Hata hivyo, Jaji Mugambi aliamua kuwa masuala yaliyowasilishwa na walalamishi hayawezi kupuuzwa, na Mahakama Kuu ina mamlaka ya kuhakikisha kuwa kila tawi la serikali linafanya kazi kulingana na katiba.
“Mahakama ina mamlaka ya kuamua mzozo huu kwa kuwa ni jukumu lake kuchunguza kama mchakato huo unakidhi viwango vya kikatiba,” alisema jaji huyo.
Miongoni mwa walalamishi waliopinga mswada huo ni Katiba (Katiba Institute), The Institute for Social Accountability, Kituo cha Kuimarisha Demokrasia na Utawala Bora, Transparency International, wakili Suiyanka Lempaa, na Tume ya Haki za Binadamu ya Kenya.
Walalamishi hao walisema kuwa Bunge liliharakisha mchakato huo na hivyo kuvunja haki za wananchi, kupoteza imani ya umma na kudhoofisha utawala wa kidemokrasia.
Walisema kuwa Bunge lilianza mchakato wa marekebisho ya katiba kabla ya kupitisha sheria muhimu ya kuongoza kura ya maamuzi.
“Mswada huu una vifungu ambavyo vinahitaji kuidhinishwa kupitia kura ya maamuzi. Kwa hivyo, Bunge linapaswa kulazimishwa kutunga sheria ya kura ya maamuzi, jambo ambalo imekosa kufanya kwa miaka 14 iliyopita,” Katiba Institute ilisema.
Wanasisitiza kuwa sheria kuhusu kura ya maamuzi ni msingi muhimu katika mchakato wa marekebisho ya katiba kwa kuwa itasimamia jinsi kura hiyo itakavyoendeshwa ikiwa mapendekezo yatatambuliwa chini ya Kifungu cha 255(1) cha Katiba.
Pia walisema kuwa NGAAF kwa sasa inatekelezwa chini ya Kanuni za Usimamizi wa Fedha za Umma za mwaka 2016.
Jaji Mugambi alisema kuwa japo mchakato wa bunge ulikuwa unaendelea, walalamishi wameonyesha hatari zilizopo iwapo mswada huo utapitishwa.
Aliongeza kuwa ilikuwa lazima mahakama iingilie kati kwa sababu kulikuwa na hatari ya katiba kufanyiwa marekebisho ya haraka na bila mwongozo ufaao.
“Ukweli kwamba mchakato huu hauna uwazi kuhusu iwapo unahitaji kura ya maamuzi au la, ni ushahidi kuwa kuna masuala ya kimsingi ya kikatiba yanayofanya kesi hii kuwa ya msingi na ya maana,” alisema jaji huyo.
Alisema kuwa kesi hiyo ina masuala mazito ya kisheria ambayo yanahitaji kuamuliwa na zaidi ya jaji mmoja.
Jaji Mugambi aliamuru faili za kesi hizo zipelekwe kwa Jaji Mkuu Martha Koome ili ateue majaji kuzisikiliza na kuziamua.