Bunge lashutumiwa kwa 'kumwadhibu' Zuleikha
Na CHARLES WASONGA
MWANAHABARI wa runinga, Janet Mbugua, ameukashifu uongozi wa bunge kufuatia kisa cha Jumatano ambapo Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kwale katika Bunge la Kitaifa, Zuleikha Hassan alifurushwa kutoka ukumbi wa mijadala kwa kuingia humo na mwanawe mwenye umri wa miezi mitano.
Kwenye ujumbe aliouandika kwenye ukurasa wake wa Facebook, Bi Mbugua ambaye huandaa vipindi katika runinga ya NTV alitaja tukio hilo kama la kuaibisha.
“Ni aibu kwamba bunge linamhukumu mama kwa sababu ya kudhihirisha uwezo aliojaliwa na Mungu wa kuzaa mtoto. Malaika huyo pia amekumbwa na unyanyapaa kuhusiana na kitendo hicho. Muhimu ni sharti tuhimize kwamba kina mama wanafaa kusaidiwa mahala pa kazi,” akasema Bi Mbugua.
Bi Mbugua ambaye ni mama wa watoto wawili wa kiume, alileza kuwa alichukizwa na kitendo hicho kwani “kinaweza kutendewa mwanamke mwingine; na hata mimi.”
“Kwa wale ambao hawana nafasi ya kuacha watoto wao kwa watu wa kuwatunza, je, tutawaadhibu kwa kuwaleta watoto wao kazini?” akauliza.
Kinyume cha sheria
Wakati wa kikao hicho Spika wa muda Chris Omulele alimwamuru Bi Hassan aondoke bungeni akisema ni kinyume cha sheria za bunge kwa mbunge yeyote kumleta mtoto bungeni.
Tukio hilo, la kwanza kushuhudiwa katika bunge la Kenya, lilitokea siku ambayo ulimwengu ulikuwa ukiadhimisha Siku ya Kunyonyesha Duniani.
Wabunge kadha walimuunga mkono Bi Hassan wakidai alinyanyaswa na kunyimwa haki ya kumnyonyesha mwanawe akiwa kazini.
Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Nairobi katika Bunge la Kitaifa, Bi Esther Passaris aliweka picha yake akinyonyesha mitandaoni.
Aliaandamanisha na maneno: “Namuunga mkono dadangu na mwenzangu mfanyakazi, Bi Zuleikha Hassan.
“Naitaka Wizara ya Afya kuthamini unyonyeshaji na ihakikisha kwua wanawake wamesaidiwa kuweza kunyonyesha majumbani mwao na mahala pa kazi,” akasema.
Mnamo Septemba 2018 Waziri Mkuu wa New Zealand Jacinda Ardern ambaye alijifungua mtoto akiwa mamlakani, aliandikisha historia kwa kumleta mwanawe mwenye umri wa miezi mitatu ndani ya ukumbi wa ambamo mkutano wa Baraza la Umoja wa Mataifa ulikuwa ukifanyika.
Kulingana na ripoti za CNN, Ardern alipigwa picha akimbusu na kumdekeza mwanawe kwa jina Neve ukumbini kando na mumewe, Clarke Gayford.
Ilikuwa ni katika mkutano wa “Nelson Mandela Peace Summit” uliohudhuriwa na viongozi na marais wa nchi mbalimbali.