Buriani Bob Collymore
ELVIS ONDIEKI na SAMMY WAWERU
MWILI wa marehemu Bob Collymore umechomwa kama njia ya kuuaga katika hafla ya mazishi iliyofanyika Jumanne katika eneo maalumu la kuteketeza maiti Kariokor, Nairobi.
Afisa Mkuu Mtendaji huyo wa Safaricom aliaga dunia Jumatatu asubuhi, Julai 1, 2019, akiwa na umri wa miaka 61 ambapo mwili wake ulipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Lee Funeral Home.
Kwenye sherehe hiyo ya kumuaga mwendazake, ni watu wa familia na wengine wachache hasa marafiki wa karibu walihudhuria.
Jumatatu mwenyekiti wa Safaricom, Bw Nicholas Ng’ang’a, alisema ibada ya kumkumbuka Collymore itaendelea kufanyika wiki hii.
Katika risala za pole kufuatia kifo kifo cha aliyekuwa afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya mawasiliano ya Safaricom Robert Bob Collymore, imeibuka kuwa alikuwa mtu wa watu.
Marehemu Collymore aliaga duni jana, Jumatatu Julai 1 baada ya kuugua kwa muda wa miaka miwili Saratani ya damu, Leukemia.
Kulingana na wandani wake na waliotangamana naye kwa kina, wanasema iwapo kuna jambo alilothamini maishani ni ‘utu’.
Utu, ni hali ya kuwa na tabia zinazolingana na hadhi ya mtu. Kadhalika, ni hali ya kuwa na ubinadamu na kujali maslahi ya mwenzio.
Wenye hulka hii hujitia katika hali ya wenzao, wanatangamana nao na kuwasaidia kwa hali na mali.
Jeff Koinange, mtangazaji katika runinga ya Citizen na ambaye alikuwa rafiki wa karibu wa Bw Collymore, anasema maelezo hayo yamemfafanua hulka zake.
“Bob Collymore alitushauri tutunze watu kama vile tungependa kutunzwa. Alisisitiza si utu wala ubinadamu kumtendea mwenzako yale hungependa kufanyiwa,” anasema Bw Jeff.
Isitoshe, kinachobainika wazi kutoka kwa wadogo wake afisa huyu alikuwa mkwasi wa heshima.
Baadhi ya wafanyakazi wake na waliopata fursa ya kipekee kukutana naye, wanammiminia sifa chungu nzima kuwa aliwaamkua kwa heshima na kuwapa motisha.
“Kila mfanyakazi aliyekutana naye alitamani kushinda naye mchana kutwa. Hangekupita licha ya kazi uliyofanya,” wanamfafanua.
Katika baadhi ya video, Bw Collymore anaonekana akinengua kiuno, kusakata densi na kuimba. Pia, nyingine iliyonaswa wakati akiwa hai anaonekana amepakata baketi ya maji na kujimwagilia kuanzia utosini.
Usawa na kutobagua
Inayotia motisha, ni katika kisa ambapo anaonekana akiwa ‘utingo’ wa basi linalohudumu mtaa fulani jijini Nairobi, akiita abiria, ishara kuwa alikuwa mtu wa watu na kutobagua yeyote.
Jeff Koinange anaendelea kueleza kwamba marehemu alitangamana na wasiojiweza katika mitaa ya mabanda kama vile Korogocho, Kariobangi na Kibera jijini Nairobi, na kuwasaidia kifedha na hata kuwainua kimaisha.
Kulingana na mtangazaji huyu ni kwamba mnamo Jumatatu pamoja na wandani wake walishinda pamoja nyumbani kwake.
Hata hivyo, anasema alilalamikia maumivu ya uti wa mgongo. “Jumamosi alifanya mazoezi kunyoosha viungo vya mwili na tukaagana kukutana mwishoni mwa wiki hii. Jumatatu asubuhi nilipokea habari za tanzia kuwa alifariki saa tisa alfajiri,” anasema Bw Jeff.
Robert Bob Collymore alizaliwa Januari 13, 1958, Guyana, Amerika Kusini. Akiwa na umri wa miaka 16 aliungana na mamake Uingereza ambako alipokea elimu.
Kuanzia 1993, Collymore alifanya kazi katika kampuni na mashirika mbalimbali ya mawasiliano ikiwamo nchini Uingereza na Japan.
Aliteuliwa afisa mkuu mtendaji wa Safaricom 2011 hadi kufikia kifo chake Julai 1, 2019.
Collymore, ameacha mke mjane, Wambui Kamiru na watoto wanne.